Polisi wa kukabiliana na ghasia walitumiwa kuwatawanya waandamanaji

Muungano mkuu wa upinzani nchini Jamhuri ya Demokrasia ya Congo unasema kuwa zaidi ya watu 50 waliuawa wakati wa mandamano ya kumpinga rais Joseph Kabila siku ya Jumatatu mjini Kinshasa.
Mmoja wa walioshuhudia anasema polisi waliwafyatulia risasi waandamanaji.

Upinzani umevilaumu vikosi vya usalama kwa kutumia risasi dhidi ya maandamano yanayotaka kutangwazwe tarehe ya uchaguzi wa urais.

Upinzani umeitisha maandamano zaidi leo Jumanne.

Waandamanaji walifunga barabara na kuteketeza magari

Serikali ya DRC iliwalaumu waandamanaji waliokuwa wamejihami na kusema waliouawa ni watu 17 wakiwemo polisi watatu.

Waziri wa mambo ya ndani Evariste Boshab amesema mmoja wa maafisa hao wa polisi aliuawa kwa kuchomwa moto akiwa bado yu hai.

Kuna wasiwasi kuwa rais Joseph Kabila ana njama ya kutaka kusalia madarakani baada ya kumalizika kwa muhula wake mwishoni mwa mwaka huu.

Mwandishi wa BBC aliyeko Kinshasa Poly Muzalia anasema polisi waliwakamata zaidi ya waandamanaji 10. 

Shule nyingi na biashara katika mji huo mkuu zilifungwa.

Kwa mujibu wa katiba, muhula wa pili wa Rais Kabila, aliyeingia madarakani baada ya kuuawa kwa babake Laurent Kabila mwaka 2001, unafaa kumalizika tarehe 20 Desemba.

Mwaka uliopita, watu 12 waliuawa katika maandamao sawa na hayo.

Tangu kujinyakulia uhuru zaidi ya miaka 55, hakuna kiongozi aliyewahi kumkabidhi mrithi wake madaraka kwa njia ya amani.

Mamia ya watu walishiriki maandamano hayo ya Jumatatu mjini KinshasaBw Joseph Kabila aliingia madarakani mwaka 2001 baada ya kuuawa kwa babake, Laurent Kabila

CHANZO: BBC SWAHILI
 
Top