Marafiki wa Kanisa la Anglikana wilayani Ngara mkoani Kagera, jana January 31,2017 wametoa msaada wa baiskeli 13 zenye thamani ya Sh 2.08 milioni kwa wanafunzi yatima wa shule ya sekondari ya kata ya Rusumo B, ili kuwapunguzia adha ya kutembea umbali mrefu kwahi masomo shuleni hapo.

Mratibu wa mfuko wa Tumaini Bw.Alex Samoya Nyamkara alisema marafiki hao wanaotoka nchini Canada na kisiwa cha Gumsey cha nchini Uingereza ambao wanafadhili miradi ya kijamii kupitia Mfuko wa Tumaini na kwamba pia wamekabidhi madaftari 1400 yenye thamani ya Sh1.6 milioni kwa wanafunzi 60 wa shule ya sekondari Rusumo B, Keza na Nyakisasa.


Bw.Nyamkara amesema kupitia wahisani hao shule 22 za kata wilayani Ngara zimenufaika kwa kuboreshewa mazingira ya kufundishia na kujifunzia hasa kwa kujengewa matundo ya vyoo , matanki ya maji na miundombinu mingineyo huku wanafunzi hao wakipatiwa taa za umeme wa jua (solar) ili kujisomea usiku.

Alisema wanafunzi waliopatiwa baiskeli hizo hutembea umbali wa kilomita 14 kwenda na kutoka shuleni na huchelewa kuanza masomo ambapo baadhi yao hasa wanafunzi wa kike huacha masomo kwa kukumbana na vikwazo vya maisha wanaopata ujauzito katika umri mdogo na kukatisha ndoto zao.

Pia alisema shule ya sekondari ya Kabanga wanafunzi wanajengewa matundu 10 ya vyoo yenye thamani ya Sh.42 milioni, Shule ya Sekondari Murugwanza, wanajengewa matanki ya maji, na wanafunzi wanaofaulu kitato cha nne na cha sita ambao ni yatima wataendelea kupewa mikopo kusomea fani mbalimbali.

“Kwa wanaojiunga na vyuo vya uuguzi na ualimu hao wanapewa mikopo asililimia 100 na wanarudisha baada ya kupata ajira na kuanza kujikimu pamoja na familia zao ili kuwawezesha kutokata tamaa ya kujiendeleza kimaisha” Alisema Nyamkara


Aidha Mkuu wa shule ya Sekondari Kabanga,Bw. Aaron Sekazoya alisema katika shule yake yenye wanafunzi yatima 54 wanaofadhiliwa na Tumaini fund walioko kidato cha tano na sita wanapatiwa sh 120 kwa ajili ya ada ya mwaka na matumizi mengineyo, ikiwa ni pamoja na fedha za mitihani kwa kidato cha nne.
Pia wanafunzi hawa hujaza fomu maalum kwa ajili ya kutaja mahitaji yao na hatimaye baadhi yao hupatiwa madaftari sare za shule na taa za kujisomea kwa wanaotoka mazingira yasiyokuwa na nishati
Alisema shuleni kwake kunafanyika ukarabati wa matanki mawili ya maji yenye ujazo wa lita 80,000 ili kukidhi mahitaji ya maji shuleni ambapo kwa siku maji yanayotumika ni kati ya lita 3,000 hadi 4,000 na kwamba shule hiyo itakuwa na wanafunzi wa bweni na kutwa 936 iwapo wataripoti wote wa kidato cha kwanza


Wakizungumza na wanafunzi waliopokea msaada baikeli na madaftari kwenye shule hizo marafiki wa kanisa hilo kutoka kisiwa cha Gamsey nchini Uingereza Sofi Danford pamoja na Linda Winey wa nchini Canada waliwataka wanafunzi kujifunza kwa bidii na kutimiza ndoto zao kupitia taaluma ya elimu.

Linda alisema pamoja na kuitembelea wilaya ya Ngara mkoani Kagera katika shughuli za kichungaji, bado watahitaji kusaidia sekta nyingine za kijamii kama kuwajengea nyumba wasiojiweza, kuelekeza misaada kwa wanafunzi wa shule za msingi ambao baadhi yao wanakosa mahitaji katika familia.

HABARI NA PICHA KWA HISANI YA SHAABAN NDYAMUKAMA


 
Top