Vugu vugu la kudai uhuru kutoka kwa mkoloni lilianza mwaka 1957/58 wakati huo Ngara ikitawaliwa na mfumo wa machifu na DC wa kikoloni (mkuu wa wilaya) aliyejulikana kwa jina la D.C Sword.
Ndugu Felix Muganga alifika Ngara kutoka Bukoba Julai 1957 akiwa na kadi za TANU billa ya ruhusa ya DC kama ilivyotakiwa wakati ule, alikwenda sokoni Nyamiaga kuwatangazia wananchi habari za TANU na juhudi zake katika kudai uhuru.

Maneno yake yaliwasisimua sana watu hivyo walikata kadi kisirisiri miongoni mwao akiwemo Ndugu Daniel Semguruka (mfanyabiashara hapo) ambaye baadae aliacha biashara yake na kuanza kueneza TANU wilayani Ngara. Alisafiri hadi Bukoba kwa Ndg Muganga ambapo alipatiwa kadi 200 za TANU na kumfanya katibu wa kwanza wa TANU wilayani Ngara.

Haikuchukua muda ndugu Semguruka na wenzake, akiwemo Ndg Taibu Songoro wa Nyakahura (wilayani Biharamulo) aliyekwisha kata kadi yake , walimwendea D.C wa Ngara ili kuandikisha tawi la TANU. DC akiwa kama ameudharau mwiba alikubali kuiandikisha TANU wilayani Ngara. Baada ya hapo viongozi waliieneza TANU kwa kasi kiasi kwamba hata wale waoga walianza kukata kadi za TANU.

Kazi ilikuwa ngumu kuhusu wapi wapate ofisi ya chama cha TANU wilayani Ngara lakini hamasa za kupenda chama na ukombozi wan chi (uhuru) zilimsukuma mwanaharakati mmoja Ndg Leonard Lukutare wa Rulenge kutoa nyumba yake ili itumike kama ofisi ya TANU na vikao na mikutano mingi ya awali vilifanyikia Rulenge katika nyumba hiyo. Baadae chama cha TANU kilipata nguvu na kuihamishia ofisi hiyo Ngara mjini kwenye nyumba ya mwanaharakati mwingine Ndg. Ibrahim Ally Mohamed.

Aidha wakoloni walipogundua kuwa TANU inaenea kwa kasi walishirikiana na machifu wa Ngara kufanya kila njama kuizuia isienee sana. Katika miaka ya nyuma sana Mwami Mwambutsa wa Burundi aliwaahi kudai kuwa Bugufi moja ya tarafa mbili za wilaya ya Ngara kuwa ilikuwa sehemu ya utawala wake.na kipindi hicho katika kikao cha maridhiano Mwami Mwambutsa aliletwa Kanazi huku amekaa kwenye kigari cha enzi zile akitaza Burundi na alipofika ardhi ya Bugufi ilinyesha mvua kubwa yenye upepo na ukungu mkubwa hali ilyosababisha ardhi ya Bugufi kutoonekana na zaidi ng’ombe zote ziliwekewa mabango yaliyosomeka DON’T LIKE MWABUTSA aidha kitendo hicho cha kudai Bugufi ni yake kuliwaudhi sana Wahangaza.

D.C wa Ngara na machifu wakielewa uzito wa chuki hiyo, walizusha uvumi kwamba viongozi wa TANU walikuwa wakiuza kadi za chama cha UPRONA cha Burundi kilichoongozwa na Prince Rwagasore eti kuifanya Bugufi iwe kama alivyodai Mwami Mwambutsa, sehemu ya Burundi. Wachache sababu kutojua kusoma waliamini na kuiona TANU kama chama kitakachowatosa utumwani. Mbinu hiyo ilishindwa.

Wakoloni hawakukubali kushindwa, walipanga na kuwalipa wahuni kwenda Mabawe kufyeka mibuni 300 katika shamba la Ndg Joel Nzobakwila na kuwakata miguu ng’ombe wake kadhaa. DC kwa kushirikiana na machifu walieneza uvumi kuwa tukio hilo limefanywa na viongozi wa TANU wakiwemo wana kamati yaani, Ndg Daniel Semuguruka, Obedi Ntiruvako, Ibrahim Ally Mohamed, Edwin Nyamubina Uria Ntamarengero. Tukio lilileta wasiwasi hadi makao makuu Bukoba wakatuma tume ili kuchunguza tukio hilo, tume hiyo akiwemo Ndg Edward Barongo ilipofika Ngara iliambiwa na chifu kuwa mkutano wa uchunguzi waufanyie nyumbani kwake ili aweze kuwalaghai lakini mbinu hiyo iligundulika baada ya kugundua kuwa pindi tukio linafanyika viongozi wote wa TANU walioshukiwa walikuwa nje ya Ngara hivyo ilionekana dhahiri kuwa chifu na DC ndio walishirikiana kufanya uharifu huo.

Mapambano yaliendelea huku kikundi cha TANU cha vijana kilichoitwa TANU YOUTH LEAGUE kikishikwa na kuteswa na hatimaye kufungwa jera ili kudhoofisha nguvu ya TANU.

Mipango mingi ilisukwa huku majungu yakichochewa dhidi ya katibu wa awali wa TANU mpaka akaondolewa kazini na nafasi yake kuchukuliwa na kijana ambaaye hakuyaelewa mazingira ya Ngara vizuri. Kijan huyo akiwa kibaraka alishirikiana na chifu kuhamisha ofisi kutoka Ngara na kuipeleka Muhweza maili kumi kutoka mjini Ngara ofisi ilipokuwa mwanzo. Kwa kuhamishia ofisi Muhweza chifu alilenga mambo matatu ya kuidhoofisha TANU; kwanza kuwadhibitishia wananchi kuwa yeye alikuwa na mamlaka na nguvu sana wilayani Ngara, pili kwa vile ofisi hiyo ilikuwa mbali na viongozi shupavu ingekuwa rahisi kwake kuivunja TANU na tatu chifu alielewa kuwa ofisi ya TANU iliandikishwa rasmi kwamba ilikuwa Nyamiaga na sio Muhweza hivyo kuwepo Muhweza kungewapa nguvu wakoloni kuipiga marufuku.

Njama hizo zilishindikana na baada ya viongozi shupavu wa TANU kugundua waliihamisha ofisi hiyo usiku na kuirudisha Nyamiaga na kuzua mgogoro uliofika Bukoba hivyo makao makuu kutuma viongozi kuja kuchunguza na hatimaye waligundua kuwa katiba wao huyo kijana alipewa rushwa ili ahamishie ofisi Muhweza.

Wakoloni walijaribu kuingiza chama cha U.T.P na Congress wwilayani Ngara ili kuiua TANU walishindwa pia walimtumia msaliti wa TANU Mzee Suleimani Takadiri aliyekuja Ngara kueneza chuki juu ya TANU na kufikia kwa Bwana Shauri Mwafrika alipewa pia sapoti ya kujieleza lakini mbinu zake zilishindwa.

Pambano la mwisho na la uamuzi likawaa mwaka 1958 ambapo Mwl Nyerere alifika Ngara na kuhutubia mkutano mkubwa sana eneo la Kanazi palepale ambapo palikuwa makao makuu ya chifu wa Ngara. Nyerere aliiongezea kasi TANU sababu ya mkutano huo huku wanachama wakiongezeka.

Baada ya Nyerere kuondoka DC Sword aliitisha mkutano na kuwahutubia wananchi akisema Nyerere ni mwongo na maneno yake ni ya upuzi mtupu na yupo kwa ajili ya kuwaibia fedha. Kauli hizo ziliwaudhi wananchi ambapo mmoja Ndg Sylivester Mdiguza alijitoa mhanga na kumwuliza DC maswali kwamba kama Nyerere ni Mwizi, mbona ameruhusiwa na serikali kuunda chama na kuchapisha kadi kutuuzia wananchi? ,na kwanni ameruhusiwa kufika hapa kutuhutubia kama kweli ni mwongo? Mzee alipandwa na hasira na kumtandika DC Sword makofi mawili hali iliyopelekea kuvunjika mkutano huo na DC hakujibu alifunga mkutano na siku nyingine aliitisha mkutano lakini haukufanikiwa.

Wahangaza wa Ngara kushirikiana na wahangaza blog tunatoa shukurani kwa hao wazee wetu waliochangia kupatikana kwa uhuru wetu ambao tunajivunia mpaka sasa baadhi wapo hai na wengine walishatangulia mbele za haki ila pongezi zetu ziwafikie wanafamilia wa wanaharakati hao.

Imechapishwa na Ezra Essau kwa kushirikiana na Essau Hosea Chiza




 
Top