Shirika la Afya Duniani (WHO), limejiunga katika
mapambano dhidi ya ugonjwa wa homa ya dengue kwa kuagiza vipimo 1,000 kwa ajili
ya upimaji nchi nzima.
WHO
imechukua hatua hiyo kusaidia juhudi zinazoendelea za kupambana na homa hiyo na
imeagiza utafiti zaidi ufanyike ili kutambua aina halisi ya virusi vya dengue
vilivyopo nchini kwa kulinganisha na vile vinavyopatikana katika maeneo mengine
duniani.
Akizungumza na gazeti hili jana, Ofisa
wa Taaluma na Udhibiti wa Magonjwa wa WHO, Dk Grace Saguti alisema tayari
chombo hicho kimeagiza vipimo hivyo vitakavyogharimu Sh17.7 milioni na kila
kimoja kinaweza kupima sampuli 25, hivyo kunufaisha watu 25,000.
Hatua hiyo imechukuliwa huku kukiwa na
taarifa kwamba baadhi ya hospitali za Serikali za wilaya na rufaa zinakabiliwa
na uhaba wa vipimo, hali iliyosababisha kutoza kati ya Sh25,000 hadi Sh30,000
kwa ajili ya kupima mgonjwa mmoja.
Katika vituo binafsi, wagonjwa wamekuwa
wakipimwa kwa gharama inayofikia Sh50,000 hadi 60,000 kwa kila mtu.
Juhudi hizo za WHO zimetangazwa siku
moja baada ya Serikali kupitia Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk
Steven Kebwe kulieleza Bunge kuwa kwa sasa vipo vipimo 350 na Serikali
inatarajia kuagiza vingine 750.
Dk Saguti alisema WHO imeshatengeneza
miongozo, mikakati na mafunzo pamoja na kutoa vitendea kazi ili kujua namna ya
upimaji na udhibiti.
“Sheria za afya za kimataifa za mwaka
2005 hadi 2007, zinaelekeza nchi kuhusu tatizo lolote lisilo la kawaida
liripotiwe WHO. Serikali ya Tanzania ilifanya hivyo na miongozo ya homa ya
dengue ikatolewa,” alisema.
Alisema miongozo iliyotolewa na WHO ni
pamoja na tatizo la dengue lisiachwe mikononi mwa Wizara ya Afya pekee, bali
sekta zote zihusishwe katika kuudhibiti.
Miongozo mingine ni uhamasishaji wa
upatikanaji wa vipimo ili kuhakikisha watu wenye dalili hizo na ambao wamepimwa
hawana malaria, wanapimwa na kutibiwa kama inavyotakiwa.
Alisema miongozo mingine ya WHO ni
kuwapo rasilimali fedha ili vituo vya afya viwe na dawa pamoja na vipimo.
Tayari Rais Jakaya Kikwete ameagiza
Wizara ya Fedha na ile ya Afya kushirikiana na Bohari Kuu ya Dawa (MSD)
kupambana na ugonjwa huo kwa dharura.
Chanzo: Mwananchi.