Mshambuliaji wa Timu ya Taifa ya Uruguay ,Luis Suarez ameibua mgogoro mkubwa huko Brazil baada kuonekana akimuuma Meno Beki wa Italia Giorgio Chiellini kwenye Mechi ya mwisho ya Kundi D la Fainali za Kombe la Dunia ambayo Uruguay waliitoa Italia kwa bao 1-0 (June 24, 2014) na wao kutinga Raundi ya Pili ya 16 bora.
Tukio hilo lilitokea Dakika chache kabla ya Bao la Kichwa la Dakika ya 81 la Diego Godin kuwapa ushindi Uruguay.
Mara baada ya tukio hilo la kung’atwa, Chiellini aliinua Jezi yake kumwonyesha Refa Marco Rodriguez wa Mexico ambae hakuchukua hatua yeyote.
Aprili 2013, Luis Suarez alifungiwa Mechi 10 kwa kumuuma Meno Beki wa Chelsea Branislav Ivanovic kwenye Mechi ya Ligi Kuu Uingereza.
Mwaka 2010 huko Uholanzi, Suarez alifungiwa Mechi 7 kwa kumuuma Kiungo wa PSV Eindhoven Otman Bakkal.
Miaka minne iliyopita huko Afrika Kusini kwenye Fainali za Kombe la Dunia Suarez alizuia Mpira uliokuwa ukitinga Golini kwenye Dakika ya 120 kwa Mkono wake na yeye kutolewa nje kwa Kadi Nyekundu, Ghana kupewa Penati ambayo Asamoah Gyan aliikosa na hatimae Uruguay kutinga Nusu Fainali kwa Mikwaju ya Penati.
Italia wametupwa nje ya Kombe la Dunia na Uruguay baada ya kufungwa Bao 1-0 huku wakicheza Mtu 10 kufuatia Kadi Nyekundu kwa Claudio Marchisio kwenye Dakika ya 60.
Mbali ya kufungwa na kupewa Kadi Nyekundu, hasira kubwa za Italia zipo kwa Refa Marco Rodriguez wa Mexico kwa kutoona Luis Suarez akimng’ata Meno Beki wa Italia Chiellini.
Bao la ushindi la Uruguay lilifungwa kwa Kichwa na Beki Diego Godin katika Dakika ya 81.
Toka Kundi D, Costa Rica na Uruguay zimesonga Raundi ya Pili ya Mtoano na Italia na England kutupwa nje.