SIKU moja baada ya mahabusu tisa wa gereza la Wilaya ya Geita mkoani hapa kugoma na kuvua nguo hadharani mbele ya Mahakama ya Wilaya, uongozi wa serikali jana ulilazimika kwenda gerezani kukutana nao.
Maofisa waliowatembelea mahabusu hao wametoka mahakama ya wilaya, ofisi ya mwanasheria wa serikali pamoja na ofisi ya upelelezi wa makosa ya jinai mkoa.
Akizungumza ofisini kwake jana, Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Geita, Desideric Kamugisha, alisema walilazimika kuchukua hatua hiyo jana na wakafanya mazungumzo na mahabusu pamoja na wafungwa kuhusiana na malalamiko yao ya kutotendewa haki.
Alisema baadhi ya malalamiko hayo ni kuchelewesha kwa upelelezi wa kesi zao hususani za mauaji na unyang’anyi wa kutumia silaha, huku baadhi ya wafungwa wakidai kuhukumiwa adhabu kubwa tofauti na makosa husika na kutokupata fursa ya kukata rufaa.
“Tumekubaliana nao na kuwataka waorodheshe malalamiko yote ambayo wameyataja mbele yetu wakiainisha namba ya shauri, mwaka pamoja na mahakama husika.
“Kazi hiyo imeanza tangu jana, kwa hiyo matokeo yataanza kujitokeza muda si mrefu kuanzia leo, ili kumaliza kero hii,” alisema.
Kamugisha alisema  kwa mujibu wa mwongozo wa kusikiliza kesi kwa mwaka, mahakama inatakiwa kusikiliza mashauri 250, lakini wamejitahidi kusikiliza kesi 436 tangu Januari hadi Mei mwaka huu, pamoja na kuwa na upungufu wa hakimu mmoja wa wilaya na wawili wa mahakama ya mwanzo.
Mkuu wa Gereza la Geita, Joseph Mbilinyi, alisema wameanza kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa katika mazungumzo hayo, ili kuondoa malalamiko hayo.
Wakili wa Serikali Mkoa wa Geita, Mwasimba Hezeroni, alisema kuwa changamoto walizopata walipotembelea gerezani humo watazifanyia kazi kwa muda muafaka, na akataka kila upande utekeleze kazi zake kwa wakati kwa maana ya mahakama, mwanasheria wa serikali pamoja na ofisi ya  upelelezi wa mkoa.
Mahabusu hao walichukua hatua hiyo juzi asubuhi  muda mfupi baada ya kutoka mahakamani bila kesi zao kusikilizwa na kulazimishwa kupanda kwenye gari ya polisi kurudishwa mahabusu.

Na  Valence Robert
 
Top