Baada ya Waziri wa Elimu na Mafunzo, Dr Shukuru Kawambwa, kuzushiwa kifo imeelezwa na ndugu zake kuwa ni mzima wa afya na anatumikia taifa.
Mapema Jumanne uliibuka uvumi kupitia baadhi ya mitandao kwamba Waziri huyo ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Bagamoyo(CCM) alikuwa amwaga dunia.
Lakini mbunge wa Chalinze, Ridhwan Kikwete akajitokeza kukanusha habari hizo kupitia ujumbe mfupi.
Ridhwan alisema: “Ndg Watanzania,WanaBagamoyo na wapenda maendeleo, kwa niaba ya CCM-Bagamoyo na Ofisi ya Mbunge-Jimbo la Bagamoyo napenda kuleta kwenu masikitiko yetu kwa niaba ya Chama na familia ya mheshimiwa mbunge Shukuru Jumanne Kawambwa kutokana na usumbufu ambao umesababishwa na habari zinazoenezwa mitandaoni kwamba mheshimiwa Kawambwa amekumbwa na umauti akiwa njiani anaelekea Mwanza,” alibainisha Kikwete.
“Mheshimiwa Shukuru Jumanne Kawambwa yupo nchini Canada akitimiza majukumu yake. Hivyo watanzania na wana Bagamoyo mnaombwa radhi kwa usumbufu uliotokea na kwamba mheshimiwa mbunge yuko na afya njema na utekelezaji wa majukumu unaendelea kama kawaida”, alikamilisha Ridhiwani Kikwete ambaye ni mbunge wa Chalinze (CCM).
 
Top