Wa kwanza kushoto OCD Bwire akiwa na viongozi mbalimbali wa ccm mkoa wa Geita katika kijiji cha nkome hivi karibuni
SAKATA la mkuu wa polisi(OCD),wilaya ya Geita(SSP)Busee Bwire kumshambulia mkewe Taus Mashaka,kwa ngumi na mateke kisha kumuuma mdomoni na kumjeruhi limechukua sura mpya baada ya mkewe huyo kumfungulia mashitaka.

Hatua ya mwanamke huyo kufungua mashitaka imekuja wakati baadhi ya vigogo ndani ya jeshi hilo walio karibu na OCD Bwire wakihaha kumnusuru mwenzao huyo ili asipandishwe mahakamani kwa kumsihi mwanamke huyo kuachana na suala hilo. 

Habari za kiuchunguzi kutoka ndani ya jeshi hilo zimebainisha kuwa jarada lililofunguliwa na mwanamke huyo ni la kudhuru mwili namba GE/RB/4946/2014 katika kituo cha polisi wilaya ya Geita.

‘’Tarehe 29/07/2014 saa 2 asubuhi huko katika kambi ya polisi Geita Sadock Bwire OCD Geita alimpiga mke wake aitwaye Taus Mashaka ambaye ni askari polisi wa kitengo cha trafiki Geita alimpiga ngumi na kumuuma meno mdomoni’’ilisomeka sehemu ya taarifa iliyofunguliwa kituoni hapo.

Imeelezwa kuwa,mke wa OCD Bwire amefikia hatua hiyo baada ya kuona hali yake kiafya bado haijatengemaa na imetokana na shinikizo la baadhi ya ndugu na jamaa ambao walimtaka kufanya hivyo kwa mjibu wa sheria kutokana na madhara ya kimwili aliyosababishiwa na mumewe huyo.

Awali kabla ya kesi hiyo haijafunguliwa dhidi ya OCD Bwire,kulikuwa na jitihada mbalimbali za kutaka kufichwa kwa suala hilo lisijulikane.

Hata kaimu kamanda wa polisi mkoa wa Geita,SSP Peter Kakamba alipohojiwa na vyombo mbalimbali vya habari hivi karibuni mbali na kukiri mwanamke huyo kujeruhiwa,alikana kumjua mtu aliyefanya kitendo hicho.

Kwa mjibu wa vyanzo vyetu kutoka ndani ya jeshi hilo vimeeleza kuwa,kwa sasa mwanamke huyo ambaye pia ni askari polisi mwenye cheo cha meja kitengo cha usalama barabarani Geita amefichwa kwenye hoteli moja ya mjini Geita akiendelea kupatiwa matibabu kwa siri lengo likiwa ni kuweka kizingiti kwa vyombo vya habari ili visiendelee kulikuza suala hilo.

Aidha tukio la OCD Bwire kumshambulia na kumjeruhi mkewe lilitokea julai 29 mwaka huu majira ya asubuhi katika kambi ya polisi Geita.

Imeelezwa kuwa,Bwire alimpiga mkewe huyo kwa ngumi na mateke kabla ya kumuuma meno mdomoni kisha kumsababishia majeraha hali iliyopelekea baadhi ya vigogo ndani ya jeshi hilo kufanya jitihada za makusudi ili kuficha suala hilo lisigundulike chanzo cha ugomvi huo kikielezwa ni wivu wa mapenzi.

Na Victor Bariety-Geita
 
Top