Mjumbe wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Profesa Palamagamba Kabudi (kulia) akizungumza kwenye mdahalo wa Katiba, uliofanyika Dar es Salaam jana (Agost 04,2014). Picha na Edwin MjwahuziNa Fidelis Butahe na Ibrahim Yamola- Mwananchi.
Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba na wajumbe wa tume hiyo, jana(Agost 04,2014) walitoa ufafanuzi wa hoja mbalimbali kuhusu mchakato wa Katiba katika mjadala uliofanyika Dar es Salaam kiasi cha kuwafanya waliohudhuria siyo tu kumshangilia, bali walimsindikiza hadi alipoingia kwenye gari lake na wakilifuata na kulisukuma.


Jaji Warioba na wajumbe wenzake, Profesa Palamagamba Kabudi, Joseph Butiku, Hamphrey Polepole, Mwantumu Malale na Awadh Ali Said walitoa ufafanuzi huo katika mdahalo la Katiba lililoandaliwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere jana(Agost 04,2014.


Jaji Warioba ndiye alianza kuzungumza kwa kukanusha madai yaliyotolewa juzi katika mdahalo mwingine, kuwa amepeleka maoni mapya serikalini.


Alisema madai hayo hayana ukweli bali maoni aliyowasilisha serikalini yalitokana na maoni ya wananchi waliyokusanya wakati wakiandaa Rasimu ya Kwanza ya Katiba ambayo yataweza kusaidia katika kuandaa Katiba ya Tanganyika.


Juzi(Agost 03,2014), katika mdahalo uliorushwa na Star TV, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi alidai kuwa Jaji Warioba amewasilisha serikalini maoni mapya, ukiacha yale ambayo yapo katika Rasimu ya Katiba.


Jaji Warioba alisema Tume iliandaa sura ya kwanza iliyohusu mali na maliasili na sura ya tano kuhusu Serikali ya Muungano na sura ya nne iliyoelezea serikali za mitaa.


“Sura ya nne na tano tulibaki nazo lakini Machi 27, mwaka huu niliandika barua kwa Waziri wa Katiba na Sheria, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Chikawe (Waziri wa Mambo ya Ndani, Mathias Chikawe) kwa kuwa alikuwa Waziri wa Katiba na Sheria kipindi hicho na nikawakabidhi ili isaidie katika mchakato wa Katiba hasa wakati wa kuandaa Katiba ya Tanganyika,” alisema Jaji Warioba.


Aliongeza; “Hayakuwa mawazo mapya wala sikupeleka mawazo mapya, bali ni mawazo tuliyoyakusanya kutoka kwa wananchi na nimeamua kufanya hivyo kwa kuwa tume kwa kipindi chote ilikuwa wazi na mimi nimeamua iwe ‘public’ (wazi) kwa kila mmoja kujua, ili iwasaidie kujua wakati wa uandaaji wa Katiba ya Tanganyika.”


Jaji Warioba pia alifafanua sababu za tume kupendekeza muundo wa serikali tatu, kwamba haikufanya hivyo kutokana na idadi ya watu waliotaka muundo huo, bali ilitizama uzito wa hoja zilizotolewa.


“Wapo wanaosema kuwa idadi ya watu waliotaka muundo wa serikali tatu ni wachache. Tulipendekeza muundo huo kwa sababu ya hoja zilizotolewa na siyo wingi au uchache wa waliotoa maoni,” alisema.


Alisema hoja ya kwanza ni Tanganyika kuvaa koti la Muungano pia akifafanua jinsi Tanzania Bara inavyoshughulikia masuala yake ya kiuchumi bila kugusa masuala hayo kwa upande wa Zanzibar.


“Leo hii mawaziri wangapi wa muungano wanaotembelea Zanzibar kukagua shughuli za maendeleo, pia kuna mgongano wa Katiba ya Tanzania Bara na Zanzibar. Pia suala la fedha nalo limekuwa na mvutano kwa muda mrefu hasa kuhusu pande hizi mbili kuwa na akaunti ya pamoja,” alisema na kuongeza.


KUSOMA ZAIDI>>> BONYEZA HAPA
 
Top