KATIBU CHADEMA GEITA AGEUKA KITUKO,AFUTA MAJINA YA WAGOMBEA KIBABE
KATIBU wa Jimbo la Geita chama cha Demokrasia na Maendeleo (chadema)Rogers Ruhega amekuwa kituko katika uchaguzi wa kata ya Kalangalala baada ya yeye mwenyewe kuanzisha zogo ukumbini na kutangaza kufuta uchaguzi wote bila kutaja sababu ya kufanya hivyo.
Mapema alianza kutangaza kuwafuta kwenye kinyang'anyiro hicho baadhi ya wagombea kwa madai kwamba wamevunja katiba bila kutaja ni vifungu gani vya katiba ya chadema vimekiukwa huku mkutano ukitaka kuvunjika kwa maamuzi hayo.
Aliyefukuzwa kwa kisingizio kuwa hana tawi analotoka ni Flora Rumanyika ambaye kadi yake ilikuwa inaonyesha ni kutoka tawi la Nyankumbu na mwenyekiti wa Tawi alikiri kuwa ni mwanachama wa tawi hilo lakini katibu wa tawi pamoja na Luhega wakasema hawamtambui kisha kumuondoa kwenye kinyang'anyiro kibabe baada ya kuhisi ni mmoja wa watu wasiokubaliana na uongozi wake wa kisultan.
Ruhega alionekana kuanza kuchanganyikiwa mapema baada ya matokeo ya awali kuvuja na kuonyesha kuwa waliokuwa wameshinda ni wajumbe wengi wanaomuunga mkono mgombea ukatibu wa Jimbo Mutta Robert na kuonyesha kuwa Ruhega anapoteza nafasi nyingi katika uchaguzi huo.
Uchaguzi huo wa kata uliitishwa kama uchaguzi wa marudio bada ya katibu huyo wa Jimbo kutangaza kuwa uchaguzi wa kata hiyo kufutwa kwa madai kwamba uchaguzi haukufuata katiba ili hali si kweli.
Wakati madai hayo yanaibuka ya kutofuata katiba,kuna barua zilizotoka kwenye matawi mbalimbali zikionyesha kuwa barua za kulalamikia uchaguzi huo ziliandikwa na wafuasi wa katibu huyo kwa ushawishi wake ili autengue na kuitisha upya ili ajipange vizuri baada ya kubaini waliokuwa wamechaguliwa walikuwa hawamuungi mkono katika uchaguzi wa Jimbo.
Inadaiwa kuwa katika mkakati huo wa kufuta baadhi ya wagombea na kufuta uchaguzi ili kuhakikisha wanapenyesha watu wake,unaratibiwa kwa msaada wa kiongozi wa Kanda Robert Bujiku anayedaiwa kuandaa njama za kumrudisha madarakani katibu huyo kwa hila.
Hata hivyo juzi baada ya katibu huyo wa Jimbo kutangaza kufuta uchaguzi huo bila sababu, wanachama wengi wa kata hiyo na kata za jirani waliokuwa wakifuatilia uchaguzi huo walijaa jazba na kuanzisha zogo kubwa na kusababisha baadhi ya wafuasi wa chadema kuanza kurusha maneno makali na kutishia kuchoma moto gari lake.
Wakati hayo yakiendelea,Katibu huyo,na wapambe wake akiwemo Neema Chozaile,Nguru Brighton walikuwa wamejifungia kwenye moja ya vyumba vya ofisi za jengo hilo lililokuwa likifanyikia uchaguzi huo wakihofia kupigwa na wanachama ambao walikuwa na jazba wakipinga katibu huyo kutumia mamlaka yake kufuta uchaguzi huo.
Wafuasi hao walitulizwa na mgombea mwenzake Mutta Robert aliyeonekana kusikilizwa na wafuasi wengi wa chadema,
Katibu huyo na viongozi wenzake walilazimika kujifungia ukumbini huo na kuita askari polisi na kuondoka hapo chini ya ulinzi mkali wa askari hao.
Hivi karibuni Ruhega amekaririwa akisema kuwa ameisha fanya mazungumzo na Chagulani mfuasi wa chama cha ACT anayeshi Mwanza kwa madai kwamba ameombwa kuhamia chama hicho.
Wanachama wengi wa chadema mjini hapa wamepoteza imani na Katibu huyo baada ya kupata tetesi kuwa ni shemeji yake na Zitto Kabwe na anajiandaa kuhamia ACT.
“Katibu amekuwa na matatizo mengi na amekuwa akikwamisha shughuli za chama na kupanga mikakati michafu ya kuleta migogoro ndani ya chama bila sababu za msingi na chama amekigawa katika makundi makundi,na sulihisho la haya yote ni kumuondoa katika nafasi hiyo na bila kumuondoa chadema haipo Geita” alisema kiongozi mmoja wa kamati tendaji ya Jimbo la Geita.
Alhamis ya wiki iliyopita vijana wa ulinzi wa chadema (Red Brigade) wakiwa na waandishi wa habari walikuta wafuasi wa katibu huyo katika Hoteli ya Wandela mjini Geita wakiwa wmekusanyika kama 50 wakinywa soda na vyakula mbalimbali na kukiri kwamba wameitwa kuweka mikakati ya ushindi.
Ruhega inadaiwa anajitengenezea njia ya ushindi kwa kuwashawishi wajumbe kwa pesa,vinywaji na chakula na kumtumia katibu wa Kanda Robert Bujiku, ambaye ni rafiki yake kutuma taarifa za uongo makao makuu ya chadema kuwa wagombea wenzake na mamluki kutoka chama cha mapinduzi (ccm).