LORI LILILOBEBA PAMBA LAPINDUKA SHINYANGA,MMOJA AFARIKI DUNIA,MAJERUHI WANNE,WALIKUWA WAMEPANDA JUU YA GARI HILO
Mtu mmoja aliyejulikana kwa jina la Rashid Juma(25) amefariki dunia papo hapo baada ya gari alilokuwa amepanda juu na wenzake likiwa limebeba pamba kuacha njia na kupinduka katika barabara ya Shinyanga kuelekea Pandagichiza katika kijiji cha Shilabela kata ya Pandagichiza,tarafa ya Mondo wilayani Kishapu mkoani ShinyangaLori hilo lenye namba za usajili T214 AGV aina ya scania lori mali ya kampuni ya Afrisian Ginnery ya Shinyanga likitoka Nindo kwenda Shinyanga mjini likiendeshwa na Justine Philemon(35) mkazi wa Majengo mjini Shinyanga,aliyetoroka baada ya ajali liliacha njia na kupinduka jana saa 2:40 asubuhi.
Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga SACP Justus Kamugisha amesema baada ya lori hilo kupinduka Rashid Juma aliyekuwa amepanda juu ya gari alifariki dunia papo hapo huku wenzake wanne wakijeruhiwa katika sehemu mbalimbali za miili yao na wote wamelazwa katika hospitali ya mkoa wa Shinyanga.
Amewataja majeruhi hao kuwa ni Daniel James(18) Philipo Charles(19)na Richard Samwel (19) wote wakazi wa Ibadakuli na Charles Peter(19) mkazi wa Kolandoto.
Amesema chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi huku akitoa wito kwa madereva na watumiaji wengine wa barabara kufuata sheria za usalama barabarani ili kuepuka ajali zinazozuilika.
Malunde1 blog