MSICHANA mmoja mkazi wa eneo la Minga katika Manispaa ya Singida (muuza duka), amenusurika kifo baada ya kumwagiwa uji wa moto na mke wa tajiri yake na kumsababishia maumivu makali kutokana na kile kinachosadikiwa kuwa ni wivu wa kimapenzi.
Muuguzi wa zamu katika Hospitali ya mkoa wa Singida, wodi namba mbili ya wanawake, Anna Sprian ameifahamishaFikraPevu kuwa binti huyo amejeruhiwa sehemu za sikio la upande wa kulia na mgongoni, ambapo amesema hali ya mgonjwa huyo inaendelea vizuri kutokana na matibabu anayoyapata hospitalini hapo.



Akizungumza na FikraPevu leo Agosti 10, 2014 kwa tabu, binti huyo Jackline Lasway (23), maarufu kwa jina la Pendo, amesema majeraha ya moto katika sehemu ya sikio la upande wa kulia na mgongoni.



Majeruhi, Jackline Lasway, akiwa amelazwa katika wodi ya wanawake katika Hospitali ya mkoa wa Singida, baada ya kujeruhiwa kwa kumwagiwa uji wa moto wakati akiwa dukani kwa bosi wake katika Manispaa ya Singida

Pendo amesema kuwa tukio hilo limetokea jana Jumamosi Agosti 9, 2014 saa nane mchana wakati akiwa dukani kwa bosi wake aliyemtaja kwa jina la, Charles Kamnde.

Amesema akiwa anaendelea na kazi zake za kuuza bidhaa mbalimbali dukani hapo, gafla alitokea mke wa bosi wake akiwa na chupa yenye uji wa moto na kuwa alimmwagia usoni ambapo baada ya kumwagiwa uji huo alitaka kujiokoa ili usimmwagikie usoni na ndipo ulimuunguza kwenye sikio la kulia na mgongoni na kuwa baada ya mke wa bosi wake kumkosa uso alitoa kisu kutaka kumchoma kifuani.

“Mimi sikuwa na ugomvi naye wala sijui chanzo cha yeye kufika dukani na kunifanyia vile jana, maana kama ni kazi mimi ninafanya kulingana na maelekezo kutoka kwa bosi wangu Chale lakini sijui kilichomfanya afikirie kunifanyia huu unyama” alisema.

Aidha, amesema katika purukushani za kujiokoa kuwa asichomwe kisu hicho, alifanikiwa kumkamata mkono mwanamke huyo na kupiga kelele za kuomba msaada ambapo watu walifika na kumwokoa baada ya muda mchache ambapo alichukuliwa na bosi wake hadi Kituo cha Polisi mjini Singida na kupewa PF3 kwa ajili ya matibabu na kupelekwa katika hospitali hiyo ambako amelazwa huku akiwa ma majeraha mwilini.

Kwa upande wake, mmiliki wa duka hilo Chale Kamnde alikiri kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa hayuko tayari kulizungumzia kwani maelezo aliyotoa binti huyo yanajitosheleza.

Wakiongea kwa nyakati tofauti na FikraPevu baadhi ya majirani wa familia hiyo, wameonyesha masikitiko yao juu ya tukio hilo na hatua ya mwananmke huyo kummwagia uji msichana huyo huku wakihusisha tukio hilo na wivu wa kimapenzi baina ya mfanyakazi huyo na mume wa mtuhumiwa.

“Kama aliona kama kuna sehemu kamkosea angemuonya au kama ameshindwa kueleweka basi angemshitaki hata polisi kwani kitu alichokifanya hakiendani na haki za binadamu kwakuwa ni kumdhalilisha huyu msichana ambaye alikuwa akifanya kazi kwa ajili ya kujipatia kipato chake na familia yake.

Kamanda wa Polisi Mkoani hapa, Geofrey Kamwela, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuwa wanamshikilia mtuhumiwa kwa mahojiano na mara baada ya upelelezi kukamilika atafikishwa Mahakamani kujibu tuhuma hizo.
 
Top