Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Tabora, Kansa Mbarouk (aliyevaa gwanda) akirudisha fomu ya kugombea nafasi ya Uenyekiti Taifa wa chama hicho. Waliomzunguka ni walinzi wake.Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Tabora, Kansa Mbarouk amejitokeza ‘kupimana kifua’ na Mwenyekiti wa chama hicho taifa, Freeman Mbowe katika uchaguzi wa ndani unaotarajiwa kufanyika Septemba 14.
Mbarouk alirejesha fomu hizo makao makuu ya Chadema jana mchana huku akikumbana na kizingiti cha kuzuiwa na walinzi kuingia ndani kurejesha fomu akiwa pamoja na waandishi wa habari na hata alipotoka nje hakutakiwa kuzungumza na waandishi hao karibu na jengo hilo.
Ili kuepusha vurugu, Mbarouk alitoka eneo hilo na kuanza kuzungumza na waandishi wa habari kwa kusema, “Hili ambalo limenipata kwa kuzuiwa nisipigwe picha wakati nikirejesha fomu nikiingia madarakani nitahakikisha narejesha usawa ndani ya chama hiki na katiba inazingatiwa.”
Aliongeza, “Jambo la pili kulifanya nitahakikisha wanachama wote ndani ya Chadema wanakuwa na haki sawa, hakuna atakayeonewa na atakayevunja katiba kwa njia zozote zile atachukuliwa hatua kali, hakuna atakayekuwa juu ya katiba ya Chadema.”
Juzi, Mbowe alikabidhiwa fomu na makada wa chama hicho na kumtaka awanie tena kiti hicho, ombi ambalo alilikubali na kufungua milango kwa wanachama wengine ‘kupimana naye kifua’.
“Nafasi bado ipo, anayetaka kupima kifua na mimi ajitokeze. Tena nawaomba viongozi wangu msizuie fomu kwa anayetaka,” alisema Mbowe ambaye ameongoza chama hicho kwa vipindi viwili vya miaka mitano mitano.
Mbarouk alisema, kulingana na katiba ya chama Mbowe amemaliza muda wake wa uongozi na anatakiwa kukiachia kiti hicho kiongozwe na mtu mwingine.
“Mimi nimekuwa mwenyekiti wa mkoa (Tabora) kwa kipindi cha miaka 10 nikaamua kuachia ili wengine waendeleze vivyo hivyo na Mbowe ameongoza kwa miaka kumi anatakiwa kuachia ngazi, na hii ni nafasi yangu imewadia kuiongoza Chadema kufika Ikulu 2015,” alisema Mbarouk.
Huku akisisitiza alisema, “Kauli aliyoitoa Mbowe ya kusema anayetaka kujipima kifua naye ajitokeze ni ya kuwatisha wanachama wasijitokeze, lakini mimi siwezi kutishika na ndiyo maana nimejitokeza kupimana naye kifua na ninajua nitamshinda kwani katiba ikizingatiwa tu hawezi kunishinda.” Uchaguzi huo utatanguliwa na wa Baraza la Vijana Taifa la Chadema, (Bavicha) utakaofanyika Septemba 10 huku Septemba 11 ukifanyika wa Baraza la Wanawake (Bawacha).
Hadi dirisha la urejeshaji fomu linafungwa jana saa 10.30 makada mbalimbali walikuwa wamejitokeza kuwania nafasi hiyo miongoni ni Daniel Madiba anayewania Mratibu Mhamasishaji taifa wa Bavicha na wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Lutiger Haule nafasi ya Ujumbe wa Kamati Kuu kupitia Vijana. Haule alisema anataka kuwatumikia vijana katika kupata haki zao na atatumia nafasi hiyo kuwapigania kwa nguvu zote katika harakati za kusaka ukombozi wa pili unaominywa na CCM.
Ushindani ndani ya Bawacha unatarajiwa kuwa kati ya Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, Mbunge Viti Maalum, Chiku Abwao na makada wengine, Lilian Wasira na Sophia Mwakagenda kwa nafasi ya mwenyekiti.
Katika hatua nyingine, nafasi ya Naibu Katibu Mkuu Baraza la Wanawake ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bawacha), imeendelea kupata wagombea baada ya Aisha Yusuf kuchukua fomu na kuirejesha kuwania nafasi hiyo.
Akizungumza katika ofisi za chama hicho zilizopo Kinondoni jijini Dar es Salaam, Aisha alisema kuwa amelazimika kuwania wadhifa huo kutokana na kuwa na uwezo wa kutosha. “Hivi sasa ukiangalia wanawake wengi bado wapo nyuma hivyo ni wakati wa kuondokana na dhana hiyo ndiyo maana nami nimelazimika kuomba nafasi hiyo,” alisema Aisha.
Alisema kuwa tangu alipojiunga na chama hicho mwaka 2007 amepata uzoefu ikiwamo kuwa Mwekahazina wa Bawacha Kata ya Saranga hivyo ameomba ngazi ya juu zaidi ili aweze kuwatumikia wananchi kwa ukaribu.
Aisha alisema kuwa ni vyema wanawake wakatambua wao ni jeshi kubwa linaloweza kuleta mabadiliko ndani ya Tanzania akieleza kwamba sasa taifa lina matatizo makubwa hivyo wanawake wanapaswa kujitokeza kwa wingi na kuchukua fomu ili kuwania nafasi mbalimbali za uongozi.
“Wanawake ni lazima tuwe jasiri ni lazima tuondokane na mifumo dume inayotukandamiza hiyo itatusaidia tupate nafasi za juu za uongozi katika uchaguzi mkuu ujao,” alisema.
Aisha alisema kuwa anaamini kuwa taifa hili litaweza kupata maendeleo zaidi ikiwa wanawake wengi watapata nafasi nyingi za uongozi.
Alisema kuwa tangu alipojiunga na chama hicho mwaka 2007 amepata uzoefu ikiwamo kuwa Mwekahazina wa Bawacha Kata ya Saranga hivyo ameomba ngazi ya juu zaidi ili aweze kuwatumikia wananchi kwa ukaribu.
Aisha alisema kuwa ni vyema wanawake wakatambua wao ni jeshi kubwa linaloweza kuleta mabadiliko ndani ya Tanzania akieleza kwamba sasa taifa lina matatizo makubwa hivyo wanawake wanapaswa kujitokeza kwa wingi na kuchukua fomu ili kuwania nafasi mbalimbali za uongozi.
“Wanawake ni lazima tuwe jasiri ni lazima tuondokane na mifumo dume inayotukandamiza hiyo itatusaidia tupate nafasi za juu za uongozi katika uchaguzi mkuu ujao,” alisema.
Aisha alisema kuwa anaamini kuwa taifa hili litaweza kupata maendeleo zaidi ikiwa wanawake wengi watapata nafasi nyingi za uongozi.