MWENYEKITI wa Baraza la Vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAVICHA), Bw. John Heche, amemtaka Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Bw. January Makamba ambaye pia ni Mbunge wa Bumbuli, mkoani Tanga, kuacha kufikiria urais kwani Watanzania hawataki Rais kijana bali wanahitaji mtu atakayeweza kuongoza nchi.
Bw. Heche aliyasema hayo katika mkutano wa hadhara uliofanyika mwishoni mwa wiki katika Viwanja vya Shule ya Msingi Sima A, Wilaya ya Bariadi, mkoani Simiyu.

Alisema Bw. Makamba hana sifa za kuwania urais kama anavyoamini kwa kutumia ushawishi wa vijana kupewa nafasi ya kuongoza nchi na kusema Watanzania wanahitaji kiongozi anayeweza kutatua kero zao.

Bw. Heche ambaye alikuwa kwenye ziara ya Oparesheni Sangara inayoendeshwa katika Mikoa ya Shinyanga, Simiyu na Mara, alisema Watanzania hawako tayari kuongozwa na Rais kijana.

"Makamba anaposema huu ndio wakati wa vijana kushika urais anapotoka kwani hana sifa hizo....nawaomba vijana jitokezeni kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapigakura ili tuweze kuiondoa CCM madarakani na kukiunga mkono CHADEMA," alisema.
 
Top