MWANAFUNZI UDSM KORTINI KORTINI KWA WIZI WA MILIONI 51.6/=
Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) pamoja na Meneja wa kituo cha mafuta cha Gudal Petrol Station cha Ubungo, Kibangu , wamepandishwa kizimbani kwa mashitaka mawili likiwamo la wizi.
Watuhumiwa hao, Meneja Saadi Mohamed (21) na mwanafunzi Edwin Mbuya (21), wote wakazi wa Ubungo-Kibangu, walipandishwa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni wakikabiliwa na mashtaka mawili likiwamo la wizi wa fedha taslimu Sh milioni 51.6 mali ya kituo hicho.
Mbele ya Hakimu Kwey Rusema, Wakili wa Serikali, Credo Rugaju, alidai kuwa katika shitaka la kwanza, washtakiwa hao walikula njama ya kutenda kosa katika tarehe na muda usiyojulikana maeneo ya Kinondoni.
Katika shtaka la pili, ilidaiwa kuwa Julai 28 mwaka huu, washtakiwa waliiba fedha taslimu Sh 51,689,500, mali ya Kituo cha Gudal Petrol Station kilichopo Ubungo Kibangu. Washtakiwa walikana na upelelezi umekamilika. Kesi imepangwa kusikilizwa Agosti 19 mwaka huu.
Katika hatua nyingine, mkazi wa Mbezi Luis, Omary Kupaza (32), amefikishwa katika Mahakama hiyo akikabiliwa na kosa la kumbaka mtoto wa miaka 14.
Mbele ya Hakimu Izhaq Kuppa, wakili wa Serikali, Masin Mussa, alidai kuwa tukio hilo ni la Desemba 2013 huko eneo la Mbezi Msigwa ambapo mshtakiwa alimbaka mtoto huyo na kumsababishia maumivu makali sehemu za siri.
Mshtakiwa alikana kutenda kosa hilo na upelelezi wa shauri hilo unaendelea. Mshitakiwa alirudishwa rumande kwa kushindwa masharti ya dhamana na kesi hiyo imepangwa Agosti 19.