Polisi wa Beijing, China hatimaye wamemkamata rasmi mtoto wa mkali waMartial Arts Jackie Chan anaefahamika kwa jina la Jaycee Chan kufuatia tuhuma za kujihusisha na dawa za kulevya.
Taarifa kutoka katika ofisi ya mwendesha mashitaka wa wilaya ya Dongcheng, zimethibitisha hatua hiyo ambapo Jaycee Chan anaweza kufungwa hadi miaka 3 jela endapo atakutwa na hatia ya kuwaruhusu watu kutumia dawa za kulevya katika nyumba yake.
Jaycee Chan alikamatwa mwezi uliopita akiwa na muigizaji mwingine wa Taiwan anaefahamika kwa jina la Ko Kai. Wawili hao walifanyiwa vipimo na kugundulika kuwa walitumia dawa za kulevya aina ya Marijuana na walikiri kuwa walipeleka nyumbani kwa Jaycee grams 100 za dawa hizo.
Kwa sheria za China, Polisi anatakiwa kuomba ruhusa ya kumkamata rasmi mtuhumiwa kutoka kwa muendesha mashitaka wa serikali. Taratibu za upelelezi zinaweza kuendelea wakati huo.
Kwa upande wa Ko Kai, alipewa kifungo cha siku 14 baada ya kukiri kutumia marijuana na baadae yeye na familia yake walifanya mkutano na waandishi wa habari na kuomba radhi kwa kitendo hicho.