Katika kile kilichoelezwa kushangaza na kuacha watu midomo wazi ni kwamba wanafunzi wa shule ya sekondari Kivukoni katika halamashauri ya mji wa Geita mkoani Geita wamepewa adhabu kali ya kuchapwa viboko wakilazimishwa kuchangia sherehe ya kuhitimu elimu ya sekondari (Graduation).
Wanafunzi hao walioongea ana Malunde1 blog ambao waliomba kuhifadhiwa majina yao kwa sababu ya usalama wao shuleni hapo walisema uongozi wa shule hiyo umetoa agizo la kila mwanafunzi kidato cha kwanza hadi 3 kulipa shilingi elfu tano kila mmoja kwa ajili ya mahafali hayo kwa nguvu wakati ilipaswa kuwa hiari.
"Juzi sisi wanafunzi wa kidato cha tatu tuliitwa na walimu wale ambao tulikuwa hatujalipa tulichapwa viboko vitano kila mmoja tukiambiwa tumegoma kutoa mchango huo"walisema wanafunzi hao.
"Sasa hivi kila mwalimu anapoingia darasani tunaitwa majina wale ambao hatujachanga tunapigwa viboko bila huruma tunawaaambia hatuna pesa tunaongezewa adhabu ya viboko vingine",walisema.
Wanafunzi hao walisema pamoja na kuchapwa viboko walitakiwa pia kuandika barua za kujieleza na hukusanywa na walimu wa madarasa kisha kupelekwa kwa mkuu wa shule huku wakitishiwa kutufukuzwa shule.
Alipotafutwa kuelezea juu ya tuhuma hizo kaimu mkuu wa shule hiyo ambaye alikataa kata kata kutaja jina lake alisema yeye hajui suala hilo na hajui kabisa kuwepo kwa mchango wa aina hiyo shuleni.
Alipoulizwa kuhusu wanafunzi kupewa adhabu wakikataa kutoa michango alikubali na kusema aliyetoa idhini hiyo ni mkuu wa shule.
Afisa elimu wa halmashauri ya mji wa Geita Cosmas Kibiti alisema kisheria inatakiwa michango iwe mekubaliwa na vikao hallali kisha kuwepo na muhutasari wa vikao tofauti na hapo ni kosa.
Na Valence Robert- Malunde1 blog -Geita