Mahakama Kuu kanda ya Dar es Salaam nchini Tanzania leo itaanza kusikiliza kesi ya msingi ya kutaka ufafanuzi wa kimahakama juu ya mamlaka na mipaka ya bunge la Maalum la Katiba iliyofunguliwa na mwandishi wa Habari Said Kubenea.
Katika shauri hilo, Kubenea anaiomba mahakama itoe tafsiri sahihi ya Mamlaka ya Bunge la Maalum la Katiba kwa kuzingatia kifungu cha 25 (1) na (2) cha Sheria ya Marekebisho ya Katiba Namba 83 ya mwaka 2011, na Pia Mahakama itamke kama Bunge hilo lina mamlaka ya kubadilisha maudhui ya Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kwa kiwango gani.
Jopo la majaji watatu likiongozwa na Jaji Augustine Mwarija, Dk. Fauz Twaib na Aloyisius Mujulizi, limekubaliana na hoja za maombi ya shauri hilo yaliyowasilishwa na wakili Peter Kibatala.
Wakati huo huo majaji hao wametupilia mbali shauri lililofunguliwa na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kupinga mwenendo wa Bunge Maalum la Katiba kwa kutokana na kutowasilishwa kwa wakati kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.