Wafuasi wa CCM na CUF jana walitwangana makonde wakigombea Uwanja wa Buguruni Chama ili kufanya mkutano wa hadhara.
Mvutano huo ulisababisha Polisi kuingilia kati na kuwatawanya wafuasi hao kisha kuwaruhusu CUF wafanye mkutano wao kwa kuwa ndiyo waliokuwa na kibali halali.
Kamanda wa Mkoa wa Ilala, Mary Nzuki alisema vurugu hizo zilidhibitiwa na Polisi waliowaondoa wafuasi wa CCM ambao hawakuwa na kibali halali.
Mashuhuda walisema ilikuwa vurugu kwa wafuasi wa CCM na CUF baada ya kupigana kwa kutumia viti na mawe na kwamba polisi walizuia vurugu hizo kwa mabomu ya machozi.
Mmoja wa viongozi wa CUF, Mohamed Mluya alisema walipewa kibali cha kufanya mkutano huo jana.
Alisema waliwaonyesha kibali chao lakini wafuasi wa CCM walionyesha kibali kilichoonyesha kuwa walipaswa kufanya mkutano Ijumaa.
Mluya alisema wafuasi hao walitaka kufanya mkutano jana bila kubadilisha kibali.