MBUNGE wa Viti Maalumu, Vicky Kamatta (CCM), amekamtwa na Polisi Mkoa wa Dodoma kwa tuhuma za kuwatumia ujumbe mfupi wa simu za matusi wabunge wenzake.Chanzo cha kuaminika kutoka mjini Dodoma kiliambia MTANZANIA kuwa kwa kipindi cha miezi kadhaa Vicky amekuwa akituma sms za matusi kwa wabunge wenzake wa viti maalumu kupitia CCM, Catherine Magige na Lucy Mayenga ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Uyui.
Taarifa zaidi zinasema kuwa wabunge hao walikuwa wakitumiwa sms za matusi kwa namba 0653 762 *** ambapo baada ya kuona hali imekuwa ikizidi waliamua kwenda kufungua jalada la malalamiko katika Kituo Kikuu cha Kati mjini Dodoma na kuomba ufanyike uchunguzi ili waweze kumbaini mwenye namba hizo.
Kutokana na maelezo hayo, Jeshi la Polisi lilianza kufanya uchunguzi kuhusu sakata hilo na kubaini namba hiyo imesajiliwa kwa jina la mdogo wa kiume wa Vicky. 
Baada ya Jeshi la Polisi kufuatilia, ilibainika namba hiyo ilikuwa ya mbunge huyo ingawa hakuisajili kwa jina lake.

Uchunguzi zaidi ukabaini kuwa sms za matusi alizokuwa anatuma, pia alikuwa akitoa taarifa kwa mwenye namba 0767 500***, akimweleza namna anavyopambana na wabunge wenzake kwa kuwatukana.

Habari zinapasha kuwa polisi wamekuwa wakifuatilia suala hilo kwa muda licha ya kuwa mara nyingi namba hiyo huwa imezimwa.

Taarifa hizo zinaeleza kuwa Septemba 28, mwaka huu polisi waliokuwa wanachunguza suala hilo walifanikiwa kuipiga namba hiyo na kupokewa.
 
Top