Mhe. Majaliwa Kasim Majaliwa

Jumla ya wanafunzi 438,960 kati ya wanafunzi 451,392 waliofaulu mtihani wa darasa la saba nchini Tanzania wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza katika shule za serikali za sekondari kwa awamu ya kwanza.
Akitangaza matokeo ya ufaulu huo kwa vyombo vya habari na wanafunzi waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia Elimu Mhe. Majaliwa Kasim Majaliwa amesema idadi hiyo ni sawa na asilimia 97.23 ya wanafunzi waliofaulu mtihani huo.

Naibu waziri, Majaliwa amesema kati ya wanafunzi waliochaguliwa wasichana ni 219,996 sawa na asilimia 97.1 na wavulana 218964 sawa na asilimia 97.28 na kuongeza kuwa takwimu hizo zinaonesha kuwa idadi ya wanafunzi waliochaguliwa imeongezeka kwa asilimia 1.08 ikilinganishwa na 96.3 ya waliochaguliwa awamu ya kwanza mwaka 2013.

Waziri Majaliwa ametoa wito kwa halmashauri kwa kushirikiana na wadau wote wa Elimu kukamilisha majengo na kuandaa mazingira ya kuwapokea wanafunzi wote waliochaguliwa kuanza kidato cha Kwanza mwaka 2015.

Pia amewahimiza wazazi, walezi, na jamii kushirikiana na uongozi wa wilaya, halmashauri, na shule kuhakikisha kwamba wanafunzi wote waliochaguliwa wanaandikishwa, na kuhudhuria hadi watakapomaliza elimu ya sekondari.

Halmashauri zilizobakiza wanafunzi 12,432 katika awamu ya Kwanza ni Dodoma, (9824) Dar es salaam (1414), Morogogoro (752), Mtwara (281) na Katavi (161) .

Waziri Majaliwa ameziagiza Halmashauri hizo kukamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa ili kuwawezesha wanafunzi hao kujiunga na Kidato cha Kwanza ifikapo mwezi Machi.

 
Top