Mbunge wa jimbo la Solwa Ahmed Salum
Vitongoji 211 katika jimbo la Solwa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga vimepita bila kupingwa kati 856 vilivyopo, baada ya vyama vingine vya upinzani kushindwa kusimamisha wagombea hivyo nafasi kuchukuliwa na chama kimoja na kushindwa kuleta ushindani kwa wanaogombea nafasi hiyo.
Hayo yalibainishwa juzi na katibu wa chama cha mapinduzi CCM wilaya ya Shinyanga Magreth Cosmas wakati akitoa taarifa kwa katibu wa mkoa wa chama hicho Maganga Sengerema, kwenye uzinduzi wa kampeni za uchaguzi wa serikali za mitaa katika kata ya Iselamagazi ,huku akiweka wazi kuwa hiyo ni dalili ya kupata ushindi wa kishindo.
Katibu huyo alisema mbali na vitongoji hivyo pia vijiji 13 kati ya 126 kwenye jimbo hilo vimepita bila kuwa na upinzani .
Katika hatua nyingine aliwataka vijana kuacha kutumiwa kama daraja na baadhi ya vyama vya siasa kuongoza maandamano na kusababisha vurugu ambazo zinaweza kufanya waishie kufungwa na kupoteza mwelekeo wa maisha.
Akizungumza kwenye uzinduzi wa kampeni mbunge wa jimbo la Solwa Ahmed Salum aliweka wazi kuwa atagombea tena katika uchaguzi mkuu ujao na kwamba wanaopita na kusema watamuangusha wanaota ndoto ya mchana
Mbunge huyo aliongeza kuwa kamwe hawezi kuachia nafasi hiyo kwa kuwa amelitoa mbali jimbo mpaka ahakikishe wananchi wanapata huduma zote muhimu.
Alisema wataendelea kuboresha huduma zote muhimu ikiwamo afya,elimu, maji ,umeme na miundombinu ya barabara ili kuwarahisishia upatikanaji wa huduma ,ambapo aliwaomba wananchi kuchagua viongozi wa mitaa,vitongoji na wajumbe wote wa CCM hatua itakayorahisisha utendaji kazi wenye tija kwa kuwa wataongea lugha moja.
Kwa upande wake katibu wa CCM mkoa wa Shinyanga Maganga Sengerema alisisitiza juu ya kuendelea kuienzi amani,upendo na mshikamano uliopo kwa watanzania na kujiepusha na vitendo viovu vitakavyoweza kuvuruga,kwani kuirudisha ni gharama kubwa iwapo wataichezea na kuwaasa wananchi kuwa makini na wanasiasa wanaotoa kauli za uchochezi.
Uchaguzi wa serikali za mitaa unatarajiwa kufanyika nchi nzima Desemba 14 mwaka huu ambao utachagua wenyeviti wa mtaa,vitongoji na wajumbe, katika mkoa wa Shinyanga tayari CCM imepita bila kupingwa katika vitongoji 456 kati ya 2761 na vijiji 70 kati ya 511 vilivyopo.
Na Kadama Malunde-Shinyanga