Shirikisho la soka barani Afrika CAF, usiku wa kuamkia hii leo lilipanga makundi na kutoa ratiba ya fainali za mataifa ya bara hilo za mwaka 2015 zilizopangwa kufanyika Equatorial Guinea kuanzia Januari 17 hadi Februari 8.
CAF walifanya shughuli ya upangaji wa makundi na ratiba ya fainali hizo huko mjini Malabo, Equatorial Guinea ikiwa ni baada ya maamuzi yaliyochukuliwa ya kurudisha nyuma kwa juma moja kwa lengo la nchi mwenyeji, kujiandaa vyema kufuatia kuchukua nafasi ya nchi ya Morocco, iliyokuwa iandae fainali hizo, lakini ilishindwa kufanya hivyo kutokana na hofu ya ugonjwa wa Ebola ambao umeyakumba baadhi ya mataifa ya Afrika Magharibi, ambako zinatoka timu nyingi.
Katika upangaji wa makundi hayo manne ya fainali za mataifa ya Afrika nchi za Equatorial Guinea, Zambia, Ghana pamoja na Ivory Coast zilipewa jukumu la kuwa vinara wa kila kundi.
Katika upangaji wa makundi hayo kundi la kwanza linaonekana kuwajumuisha wenyeji Equatorial Guinea, Burkina Faso, Gabon na Congo Brazzaville
Kundi la Pili: Zambia, Tunisia, Cape Verde, DR Congo
Kundi la tatu; Ghana, Algeria, South Africa, Senegal
Kundi la Nne; Ivory Coast, Mali, Cameroon, Guinea
Tayari wadadisi wa soka barani Afrika pamoja na ulimwenguni kote wamelizungumzia kundi la tatu na la nne kuwa makundi ya kifo kutokana na kusheheni kwa timu nguli barani humo.
Kwa upande wa ratiba inaonyesha wenyeji Equatorial Guinea watacheza mchezo wa ufunguzi dhidi ya Congo Brazzaville.