Kamanda wa polisi mkoani Tanga Frasser Kashai

Baadhi ya wakazi wa Handeni mkoani Tanga wameandamana kulaani mauaji yaliyofanywa na watu wasiojulikana baada ya kuvunja nyumba moja na kupora mali, kisha kumuua kijana aliyekuwa ndani ya nyumba hiyo.
Watu wanaosadikiwa kuwa majambazi wamevunja nyumba na kupora mali mbalimbali kisha kumnyonga mwanafunzi Isihaka Beda wa darasa la saba shule ya msingi Jitegemee iliyopo makao makuu ya wilaya ya Handeni hatua ambayo imesababisha majonzi makubwa kwa wakazi wa wilaya hiyo.

Maandamano na vilio vya wakazi wa wilaya ya Handeni kufuatia watu wasiojulikana kuvunja nyumba ya mkazi mmoja Abida Zubeir wa eneo la Kivesa lililopo makao makuu ya wilaya ya Handeni ambapo wanadaiwa kuvunja na kuiba TV, Deki, Godoro na vifaa vingine mbalimbali kisha kumnyonga mwanafunzi beda kwa kutumia mti wa kitanda cha miti wakati alipokuwa akipiga mayoe.

Kufuatia hatua hiyo baadhi ya makundi ya wazee na viongozi wa mitaa wa wilaya ya Handeni wameiomba serikali kuhakikisha wanawatumia baadhi ya vijana kusaidiana kufichua wahalifu ambao wanaishi nao katika jamii ili kupunguza kasi ya vitendo vya mauaji ya kutisha yanayotishia usalama wa wananchi.

Kamanda wa polisi mkoani Tanga naibu kamishna wa jeshi la polisi Frasser Kashai amethibitisha kutokea kwa tukio na amewaomba wananchi wa wilaya ya Handeni na mkoa wa Tanga kwa ujumla kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi ili kuhakikisha kuwa vitendo hivyo vinakomeshwa.
 
Top