Abiria wakiingia ndani ya ndege.
Mastaa kutoka tasnia ya uigizaji Bongo, Kulwa Kikumba ‘Dude’, Lucas Mhuvile ‘Joti’, Emmanuel Mgaya ‘Masanja Mkandamizaji’, Isaya Mwakilasa ‘Wakuvwanga’, Alex Chalamila ‘Mac Regan’, Sekioni David ‘Seki’ na abiria kibao wamenusurika kufa katika ajali ya ndege.
Kwa mujibu wa shuhuda wetu ndani ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, tukio hilo lilijiri asubuhi ya Alhamisi iliyopita uwanjani ambapo ndege waliyopanda ya Shirika la Ndege la Fastjet aina ya FN 141 Airbus ilipata hitilafu kwenye injini ya kushoto ilipokuwa ikiruka.
Akizungumza kwa njia ya simu na gazeti hili muda mfupi baada ya tukio hilo baya, Dude alisimulia mkasa huo kwamba, ndege hiyo ilikuwa kwenye spidi ikipaa angani ndipo ikafeli na kuanguka.
Dude alisema taarifa zilizopatikana baadaye zilidai kwamba kabla ya kuruka, ndege aina ya kunguru aliingia kwenye injini ya kushoto na ndiye aliyesababisha hitilafu hiyo kisha ndege ikakosa mwelekeo na kuserereka chini.
Kulwa Kikumba ‘Dude’.
Alisema wakati inaserereka ilikwenda kutua kwenye majani ambapo waliokolewa na fire (zimamoto).
Baada ya abiria hao kuokolewa, waliwekwa kwenye chumba maalum kutokana na baadhi yao kutaharuki na kupandwa na presha.
“Tunamshukuru Mungu tumepona maana ajali ilikuwa mbaya sana.
“Tulikuwa tunaenda Mwanza kisha mimi nitaenda Bukoba na akina Masanja wataelekea Mara kwa shughuli za kisanaa.
Emmanuel Mgaya ‘Masanja Mkandamizaji’.
“Hapa mimi niko sawa ila wenzangu hawajiwezi kwa presha,” alisema Dude.
Habari zilizopatikana baadaye zilisema kuwa wasanii hao na abiria wengine walipatiwa ndege nyingine wakaendelea na safari.
Juhudi za kumpata msemaji wa Fastjet, Lucy Mbogoro ili azungumzie ajali hiyo hazikuzaa matunda baada ya simu zote, ya ofisini na kiganjani kuita bila kupokelewa.
Chanzo Global