Haya ni majeraha yanayotokana na shambulizi alilopokea mwananchi huyu kutoka kwa askari Magereza wa Gereza la Shinyanga
KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida mkazi wa kijiji cha Nhelegani manispaa ya Shinyanga ameshambuliwa kwa kipigo na askari wa Jeshi la Magereza na kujeruhiwa vibaya sehemu mbalimbali za mwili wake baada ya kugoma kuwapa askari hao soda na biskuti.

Tukio hilo la aina yake limetokea katika Gereza la wilaya ya Shinyanga wakati mwananchi huyo aliyejitambulisha kwa jina la Lugenzi Maguta (45) alipokwenda kumsalimia ndugu yake aliyeko mahabusu aliyemtaja kwa jina la Mahushi Nangale.

Mbali ya kushambuliwa kwa kipigo hadi kupasuka katika miguu yake yote miwili kutokana na kupigwa virungu bado askari magereza hao wanadaiwa kumgeuzia kibao kwa kumfungulia shitaka la kufanya fujo gerezani tuhuma ambazo alidai ni za uongo kwa vile hakuna fujo yoyote iliyotokea.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati akipatiwa matibabu katika hospitali ya serikali ya mkoa wa Shinyanga, Maguta alisema askari waliomshambulia waliokuwa wamevaa kiraia hawakuwa zamu bali walikuwa nje ya gereza waliamua kumshambulia kwa madai walichukizwa na kitendo chake cha kukataa kuacha soda na biskuti alizokuwa nazo.

 
Top