Rais Jakaya Mrisho Kikwete ametengua uteuzi wa waziri wa ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi Prof. Anna Tibaijuka kutokakana na makosa ya ukiukwaji wa maadili ya utumishi wa umma hasa namna alivyopokea sehemu ya fedha za malipo ya Escrow huku akimweka kiporo waziri wa nishati na madini Muhongo Sospeter Muhongo.
Rais Kikwete ameyasema hayo jijini Dar es salaaam alipokuwa akizungumza na wazee wa jiji hilo ambapo amesema serikali haina upungufu wa dhamira kwa yote yenye utekelezaji wa maazimio ya bunge ambapo amesema yanayohusu utekelezaji yatatekelezwa na yanayozungumzika yatazungumzwa.
Kuhusu suala la kumwajibisha waziri wa nishati na madini Prof Sospeter Muhongo rais Kikwete ameagiza uchunguzi ufanywe na bado hajapata majibu ila ndani ya siku mbili hizi atafanya maamuzi baada ya kujiridhisha ili uamuzi atakaoutoa usiwe wa kumuonea yeyote.
Aidha rais Kikwete katika hotuba yake hakusita kuwapongeza wabunge wote kwa kazi nzuri waliyoifanya na kwamba atamshangaa mbunge yeyote wa CCM ambaye alikuwa anatetea suala la Escrow.
Akizungumzia suala la uchaguzi wa serikali za mitaa ameeleza kuridhishwa na hatua zilizochukuliwa na waziri wa tamisemi Hawa Ghasia kuhusu watendaji waliohusika kuvuruga uchaguzi huku akiliagiza jeshi la polisi kuwachukulia hatua watu wote waliohusika na vurugu wakati wa zoezi hilo kwani mtindo huo wa vurugu ukiachwa uendelee utaleta athari kubwa katika uchaguzi mkuu ujao.
Awali akimkaribisha rais ,mkuu wa mkoa wa Dsm Bw.Said Meck Sadiq amesema uchaguzi wa serikali za mitaa umefanyika kwa utulivu ambapo CCM imeshinda kwa asilimia 75, Chadema asilimia 14, CUF asilimia 11 ambapo amesema kwa matokea ya uchaguzi huo CCM bado inakubalika kwa wananchi.