Watu 18 wamejiua kwa kujinyonga katika wilaya ya Ngara mkoani Kagera kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo hasira na kukata tamaa ya maisha.
Viongozi wa dini wameshauriwa kushirikiana na serikali kuwaelimisha waumini wao ili kupunguza matukio ya namna hiyo kutokea mara kwa mara katika jamii.

Mkuu wa mkoa wa Kagera, John Mongella, alisema kufuatia matukio hayo jamii hususani viongozi wa madhehebu ya dini wanatakiwa kuwafundisha waumini wao kujiua ni dhambi.

Mongella alisema taarifa aliyopewa inaonyesha kuanzia Aprili hadi Desemba mwaka huu, watu 18 wamejiua kwa kujinyonga katika wilaya hiyo kiwango ambacho ni kikubwa.

“Watu wanajinyonga kutokana na hasira, hivyo viongozi wa dini lazima mtusaidie kuondoa tatizo hili kupitia mahubiri mnayoyatoa kwa waumini wenu maana inawezekana watu wanafanya hivyo kutokana na kukata tamaa ya maisha,” alisema Mongella.

Alisema watu wengi wanakata tamaa katika jamii kutokana na ‘kunigwa’ na hasira za kuyakatia tamaa maisha, hivyo viongozi wa dini wanatakiwa kugundua hili na kuwaelimisha waumini wao kuepukana na dhambi hiyo.

“Lakini kwa nini iwe Ngara tu na sio kwingine, lazima kuna sababu ya kufanya hivyo, afisa maendeleo ya jamii unatakiwa kuzungumza na wananchi wako,” alisema.

Mongella alisema inatakiwa wananchi kuelimishwa na kupewa moyo hasa wanapoonekana kukata tamaa ya maisha, washauriwe namna wanavyoweza kuzalisha kipato kwa tija, ili kuondokana na ukatishwaji tamaa hadi kufikia uamuzi huo mgumu.

Chanzo:Nipashe

 
Top