Serikali imesisitiza kuwa haitakuwa na msamaha kwa viongozi na watendaji ambao wametajwa kwa namna moja au nyingine kushiriki katika uchotwaji wa mabilioni ya fedha katika akaunti ya Tegeta Escrow kitendo ambacho kimesababisha serikali kupoteza mabilioni ya fedha kama kodi.
Naibu Waziri wa fedha Mh Mwigulu Nchemba ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM Tanzania Bara, amesema hayo mjini Musoma wakati akihutubia mkutano wa hadhara baada ya kuwaapisha makamanda na manaibu makamanda wa umoja wa vijana wa CCM wilaya na mkoa wa Mara, ambapo amesema lazima hatua kali za kinidhamu, kimaadili na kisheria zichukuliwe kwa wahusika wote kama ilivyoazimiwa na bunge la jamhri ya muungano wa Tanzania.
Hata hivyo Naibu huyo Waziri wa Fedha amekiri kuwa katika zoezi la ubinafsishaji wa mashirika ya umma hasa katika sekta ya viwanda serikali ilifanya makosa makubwa katika zoezi hilo kwa kuwapa watu ambao wengi wao wamekiuka mikataba ya uendeshaji wa viwanda hivyo hatua ambayo imesababisha viwanda vingi kushindwa kufanya kazi na kufanya vijana wengi sasa kukosa ajira huku serikali ikikosa kodi kupitia viwanda hivyo.
Kwa upande wake mjumbe wa halmashauri kuu ya taifa wa Chama Cha Mapinduzi Vedastus Mathayo, ameishukuru serikali kwa kukubali kutekeleza mradi wa maji wenye thamani ya zaidi ya bilioni 50 ambao amesema kukamilika kwake kutaondoa kabisa tatizo la maji kwa manispaa ya Musoma pamoja na kukubali kugharimia ujenzi wa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Mara katika eneo la Kwangwa.