Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Shinyanga mjini Kanali mstaafu Tajiri Maulid akizungumza na waandishi wa habari(hawapo pichani) wakati akitoa tamko la Chama baada ya UVCCM Kufunga ofisi za Chama hicho.
Tamko la Chama
Kamati ya siasa ya halmashauri kuu ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) wilaya ya Shinyanga Mjini mkoani Shinyanga imesema inafuatilia na kuchunguza ili kuchukua hatua kali kwa mtu yeyote aliyehusika kupanga na kutekeleza kile ilichokiita Uasi wa baadhi ya vijana wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa CCM wilaya hiyo waliofunga ofisi za chama wakishinikiza baadhi ya viongozi waondolewe kwa madai kuwa ni wasaliti wa chama.
Akitoa tamko la kamati hiyo jana kwa waandishi wa habari mwenyekiti wa CCM wilaya ya Shinyanga Kanali mstaafu Tajiri Maulid alisema CCM inalaani na imepokea kwa masikitiko makubwa juu ya jaribio la baadhi ya vijana wa UVCCM kufunga ofisi kwa lengo la kuwazuia viongozi kuingia ofisini kwa madai mbalimbali.
Tamko la kamati hiyo linakuja siku moja baada ya baadhi ya vijana wa UVCCM kufunga ofisi za CCM wilaya wakishinikiza katibu wa wilaya Charles Sangula,katibu wa siasa na uenezi wa wilaya Charles Shigino na mchumi wa wilaya ya hiyo Ahmed Mapalala waondolewe katika chama.
Vijana hao walidai hawawataki viongozi hao, kwani wamekuwa wakikiuza chama na kuwapa nafasi wapinzani, huku wakiwatolea kauli mbaya na kuwazarua umoja huo wa vijana(UVCCM), hali ambayo wanahofia kukosa viti vingi vya uongozi katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Akitoa tamko hilo Mwenyekiti huyo wa CCM wilaya alisema wanalaani uasi huo na kudai kuwa kamati yao haiamini kama kitendo kilichofanywa na vijana hao ni makubaliano ya UVCCM wilaya ya Shinyanga Mjini bali ni tamko la watu binafsi.
“Ofisi ni mali ya taasisi siyo mali ya mtu kwa hiyo kufunga ofisi maana yake huduma zisizitolewe,wao wametoa tamko binafsi,vikao vyetu vitaona nini kifanyike juu yao,hawawezi kutoa tuhuma na kutoa adhabu,hii siyo sawa,adhabu zinatolewa kwenye vikao vya chama,siyo kwa kundi la watu na kukutana na kuanza kuropoka”,alisema Maulid.
“Kutoa tuhuma ni sawa,lakini njia waliyotumia siyo sahihi,madai yao yanahitaji uchunguzi ndiyo maana sisi kama chama tunakaa vikao kwa ajili ya uchunguzi,kamati ya siasa ya halmashauri ya kuu ya chama imeelekeza kwa mwanachama yeyote ambaye atakuwa na tuhuma kwa kiongozi yeyote afuate taratibu za kutumia vikao si vinginevyo”,aliongeza Maulid.
Hata hivyo alisema tayari vijana hao 24 waliofunga ofisi za Chama wameandika barua wakielezea madai yao na kwamba uongozi wa CCM wilaya unaendelea na uchunguzi juu ya madai yao na watatoa taarifa mara tu watakapokamilisha uchunguzi wao.
Katika hatua nyingine alisema kamati yao inaendelea kufanya uchunguzi juu ya tukio la vijana hao kumshushia kichapo diwani wa Kata ya Ndala katika manispaa ya Shinyanga George Sungura(CHADEMA) aliyekatisha katika ofisi za CCM wilaya ya Shinyanga Mjini.
“Mimi sikuwepo wakati tukio hilo linatokea,lakini mpaka sasa hatujapokea malalamiko yoyote kutoka kwa diwani huyo,hata hivyo sisi kama chama tunafanya uchunguzi ili kujua undani wa tukio hilo”,aliongeza Maulid.
Na Kadama Malunde-Shinyanga