Kaimu Meneja wa vipimo mkoa wa Shinyanga Nyagabona Mkanjabi akionesha mmoja kati ya mifuko ya unga uliochakachuliwa uzito wake katika kiwanda cha nafaka Gradi Super Sembe wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake-picha na Marco Maduhu-Shinyanga
Kaimu Meneja wa vipimo mkoa wa Shinyanga Nyagabona Mkanjabi akiwa amebeba mfuko ambao uzito wake hauendani na uzito ulioandikwa juu ya mfuko-picha na Marco Maduhu-Shinyanga
Mkurugenzi wa kiwanda cha nafaka Gradi Super Sembe cha mjini Shinyanga, Dickson Msula, akizungumza na waandishi wa habari ambapo alikiri mizani zake kuchukuliwa na wakala huyo wa vipimo kwa madai kuwa zimechezewa-picha na Marco Maduhu-Shinyanga
Mmoja wa wafanyakazi wa kiwanda cha nafaka Gradi Super Sembe cha mjini Shinyanga akiendelea na kupima nafaka kwa kutumia mizani ya kiwanda cha jirani/mizani ya kuazima baada ya mizani yao kuchukuliwa na wakala wa vipimo Shinyanga
-picha na Marco Maduhu-Shinyanga
Mfanyakazi wa kiwanda cha nafaka Gradi Super Sembe akipima nafaka kwa kutumia mizani ya kuazima-picha na Marco Maduhu-Shinyanga
Ofisi ya wakala wa vipimo mkoani Shinyanga, imekizuia kiwanda cha nafaka cha Gradi Super Sembe kinachofanya shughuli zake mjini Shinyanga kuacha kutoa huduma yake kwa wananchi kwa muda, kutokana na mizani zake kutokuwa sahihi ambazo zimechezewa kwa lengo la kuwaibia wateja wanaonunua bidhaa za kiwanda hicho.
Tamko hilo limetolewa juzi na kaimu Meneja wa vipimo mkoani humo, Nyagabona Mkanjabi wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, kufuatia ukaguzi wa vipimo walioufanya kwenye viwanda vya nafaka mjini Shinyanga na kukibaini kiwanda cha Gradi Super Sembe mizani zake kuwa zimechezewa.
Mkanjabi alisema wakiwa kwenye ukaguzi huo wa vipimo, walipofika kwenye kiwanda hicho cha nafaka na kuzikagua mizani walibaini kuwa vipimo vyao havipo sahihi na wamekuwa wakiwaibia wananchi kwa kuwapunja kilo, na kuamua kukisimamisha kutoa huduma kwa muda.
“Tulipofika kwanza kwenye kiwanda hicho kukagua mizani zao, walituzuia tena ukawa ugomvi mkubwa, lakini kutokana na mujibu wa sheria, walikubali kupima ambapo tulibani kuwa vipimo vyao havipo sahihi wamekuwa wakifanya wizi mkubwa kwa wateja wanaonunua bidhaa zao”, alisema Mkanjabi.
“Ukiangalia mfuko wa unga wa sembe uliokwisha fungwa umeandikwa una kilo 5, lakini ukiupima mfuko huo una kilo 4, kamili, na pia tulijaribu kupita kwenye maduka wanaowauzia wateja wao na kutoa huduma kwa wananchi, tukabaini madudu yale yale, tulichokifanya tumezuia kiwanda hicho mpaka pale taratibu za kisheria zikakapofuatwa”,aliongeza.
Kwa upande wake mkurugenzi wa kiwanda hicho cha nafaka Gradi Super Sembe, Dickson Msula, alikiri mizani zake kuchukuliwa na wakala huyo wa vipimo kwa madai kuwa zimechezewa, huku akikanusha kuwa bidhaa zake zipo kwenye vipimo sahihi na hazina upungufu wowote.
Hata hivyo Msula alisema agizo lililotolewa na wakala huyo la kusitishwa kiwanda chake kutoa huduma kwa muda, hakubaliani nalo, licha ya kuchukuliwa mizani zake ambapo ataazima mizani kwa viwanda jirani ili kuendelea na shughuli zake, kwa kuhofia kupata hasara zaidi.
Na Marco Maduhu-Malunde1 blog Shinyanga