Watoto mapacha walioungana enzi za uhai wao, siku 2 baada ya kuzaliwa

Watoto mapacha wa kike waliozaliwa katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Mara iliyopo mjini Musoma wakiwa wameungana sehemu ya kifua na tumbo wamefariki dunia jana majira ya saa 9.10 Alasiri wakiwa katika hospitali ya rufaa ya Bugando jijini Mwanza kabla ya kufanyiwa upasuaji.
Watoto hao pacha walizaliwa Januari 4 mwaka huu na mama mmoja mkazi wa manispaa ya Musoma Helena Paulo wakiwa na uzito wa kilo 4.6 na kisha kusafirishwa hadi katika hospitali ya rufaa Bugando kwa ajili ya uchunguzi zaidi ikiwa ni pamoja na kuangalia uwezekano wa kufanyiwa upasuaji wa kuwatenganisha.

Dk. Shukuru Kibwana ambaye ni daktari katika wodi ya watoto ya hospitali ya rufaa Bugando, amesema timu ya madaktari wa upasuaji na wataalamu wengine wamefanya kila lililowezekana kuokoa maisha ya pacha hao walioungana lakini haikuwezekana.

Ameongeza kuwa kabla ya upasuaji, mapacha hao walitakiwa kupitia tomografia ( CT ) na kufanya kipimo cha Ultra Sound ili kujua kama watoto hao wameungana baadhi ya maeneo na viungo muhimu.

Dkt. Kibwana amesema watoto hao licha ya kuungana, madaktari bingwa wa hospitali hiyo wamegundua kuwa viungo vyao vingi vya mwili vilikuwa vikijitegemea, kila mmoja alikuwa na figo yake, ini na moyo wake.

Muuguzi wa zamu katika wodi ya watoto Sembosah Hiza akieleza kuwa hali ya pacha hao ilianza kubadilika jana mchana jambo lililokwamisha rufaa yao ya kwenda hospitali ya taifa Muhimbili kwa ajili ya vipimo zaidi na uchunguzi.

Agosti 6 mwaka jana mkazi wa Katoro wilayani Geita Neema Luswetura alijifungua watoto wakiwa wameungana sehemu ya kifua na tumbo wakiwa na uzito wa kilo 5.1 hata hivyo walifariki muda mfupi baadaye.

Mwishoni mwa mwaka jana hospitali ya Apollo nchini India ilitangaza kufanikiwa kutenganisha mapacha waliokuwa wameungana kutoka Tanzania katika upasuaji uliochukua saa 11 na wataalamu 50.

 
Top