Matatizo katika uzalishaji wa mbegu za kiume inahusiana na kutokuwepo kwa mbegu za kiume kwenye manii au uwepo wa mbegu kidogo sana katika manii. Mbegu za kiume huwa zinachunguzwa kwa kutumia kifaa maalum au darubini katika maabara, kwa kawaida mwanaume ili aweze kumpa mwanamke mimba anatakiwa atoe kiasi cha mbegu kati ya milioni ishirini hadi milioni mia tatu hamsini kwa tendo, chini ya milioni ishirini huwezi kumpa mimba mwanamke.

Endapo kiwango cha mbegu zitakuwa kidogo kitaalam hali hiyo huitwa ‘Oligospermia’ na kama huna kabisa mbegu hali hiyo huitwa ‘Azoospermia.Dalili za kutokuwa na mbegu za kiume

Hakuna dalili za moja kwa moja kusema kwamba utaumwa kitu fulani, lakini dalili zifuatazo huambatana na tatizo hili; kwanza ni kukaa katika mahusiano kwa kipindi kisichopungua mwaka mmoja lakini mwenzi wako hapati mimba, kushindwa kufanya tendo la ndoa kwa uume kukosa nguvu’ Low sex Drive’ na ukisimama unashindwa kuendelea na kumalizia tendo ‘Erectile dysfunction’ pamoja na kuwahi kumaliza tendo la ndoa.

Maumivu na uvimbe wa korodani, kupungua kwa vinyweleo na ndevu kutoota pia ni dalili inayoashiria matatizo ya uzazi kwa mwanaume kwani ni ishara ya upungufu wa Kromozomu au homoni za kiume.

Hizo zote ni dalili kuu za matatizo ya uzazi kwa mwanaume.

Wakati gani wa kumuona daktari?

Endapo umekaa na mwenzio mwaka mmoja au zaidi, mnafanya tendo la ndoa bila kinga yaani kizuizi chochote wakati wa kupangilia ujauzito lakini mimba haipatikani.

Kama una matatizo ya nguvu za kiume au unawahi kumaliza tendo la ndoa. Unakosa hamu ya kufanya tendo la ndoa au uume unalegea wakati wa tendo pia ni mojawapo ya chanzo.

Unakuwa na maumivu ya korodani au korodani kuvimba, maumivu ya uume na maumivu wakati wa kukojoa au uwepo wa kivimbe katika uume.
Chanzo cha tatizo

Uzalishaji wa mbegu za kiume unafuatana na ubora wa korodani kama haina tatizo lolote na kiwango bora cha mfumo wa homoni mwilini mwake. Homoni zinadhibitiwa katika ubongo na kuimarisha korodani zizalishe mbegu.

Mbegu zikishazalishwa, husafirishwa na mirija midogo sana na laini hadi katika tezi dume’Prostate gland’ ambayo kazi yake kubwa ni kuzalisha manii.

Matatizo katika mbengu za kiume ni kutokuwepo kwa mbengu kunakosababishwa na hitilafu kwenye korodani, kuzalisha mbegu zenye kasoro, mbegu zisizo na kiasi na mbegu chache.

Matatizo ya korodani husababishwa na joto kali katika korodani, maambukizi katika korodani na uume na kuumia korodani.

Mishipa ya damu kulalia korodani ‘Variocele’ pia ni mojawapo ya tatizo kubwa la kuziba kwa mirija ya usafirishaji mbegu hizo.

Zipo pia sababu za kimazingira zinazoathiri uzalishaji wa mbegu za kiume mfano kemikali za viwandani, rangi za viwandani au majumbani, dawa za mashambani na za kuua wadudu, mionzi ya X- Ray, kukaa kwenye joto kali, kuvaa nguo za kubana na kukaa mahali kwa muda mrefu, kupakata kompyuta ‘Lap top’ kwa muda mrefu, matumizi ya sigara, bangi na madawa mengine ya kulevya kwa muda mrefu na ulevi uliokithiri. Uzito mkubwa wa mwili na matatizo ya akili.

Uchunguzi.

Uchunguzi wa tatizo hili hufanyika katika hospitali za mikoa na wilaya kwa madaktari wa masuala ya uzazi.

Vipimo vya damu kuangalia mwenendo wa mfumo wa homoni mwilini Kipimo cha Ultrasound kuangalia korodani yako kwa ndani.

Uchunguzi hufanyika kisayansi hospitali tu, hakuna vifaa vingine vya kuchunguza kwa kubahatisha, unatakiwa utolewe damu, na utoe mbengu zako za kiume baada ya kupumzika kufanya tendo la ndoa angalau kwa siku tatu.

Matibabu na ushauri.

Hufanyika baada ya uchunguzi ambapo daktari atatoa dawa kuzingatia na tatizo lililopo.

Kama hakuna mbegu zipo chache au kuna maumivu au kasoro zozote.Uwepo wa kasoro za viungo vya uzazi pia ni tatizo mfano, uume mfupi, kutokuwa na korodani au kuwa na korodani moja. Wahi hospitali kwa uchunguzi na tiba.

Source: Global Publisher

 
Top