Askari wa Jeshi la Polisi amejeruhiwa na madereva wa pikipiki maarufu kama bodaboda katika fujo zilizoibuka juzi jioni katika eneo la Mzinga, Kongowe Mbagala nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam katika Manispaa ya Temeke. Akizungumza kwa njia ya simu kuhusiana na tukio hilo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Temeke, Kihenye Kihenya alisema askari walikuwa kwenye doria kwa kutumia pikipiki maarufu kama Tigo na walipofika eneo la Mzinga walimkamata dereva mmoja aliyebainika kuwa na matatizo kadhaa kwenye pikipiki yake.

“Polisi walimkamata mwendesha pikipiki mmoja na ikabainika kwamba alikuwa na makosa kadhaa ambayo yalimpasa alipe faini. Lakini madereva wenzake walipoona amekamatwa wakaanzisha fujo na kumjeruhi mmoja wa askari kwa kumpiga chupa usoni,” alisema Kihenya.

Aliongeza kuwa “Tumekamata bodaboda kumi na tano na tayari tunaendelea na uchunguzi ili kuweza kubaini wahusika wakuu na tuweze kuwafikisha mahakamani kwa kosa la shambulio,” alieleza.

Mashuhuda wa tukio hilo walisema fujo hizo zilikuwa kubwa kiasi kwamba polisi walilazimika kuwatawanya washambuliaji kwa kupiga risasi za moto hewani.

“Mimi nilifunga duka nikakimbia maana kulikuwa hakukaliki hapa, walipompiga yule askari, uso wote ulitapakaa damu ndipo wakarusha risasi hewani. Kila mtu alikimbilia anakojua mwenyewe,” alisema moja wa mashuhuda aliyeogopa kutajwa jina lake.

Kwa upande wake, Sanja Justin, alisema yeye alikuwa ana safari ya kwenda Mbagala na alipokaribia kituoni cha basi, alisikia mlio wa risasi na kuamua kukimbia na kurudi nyumbani.

“Nilitaka kwenda kupanda gari nielekee Mbagala lakini nilipofika karibu na kituo nikasikia mlio wa risasi, nikarudi mbio na kila mtu alikuwa kwenye harakati za kukimbia ili kujiokoa na matatizo,” alisema.

Eneo la Mziga limekuwa na matukio mengi ya kihalifu ambapo mwishoni mwa mwaka jana kuliibuka kikundi cha kihalifu kilichojiita Black Amerika na kusababisha ukosefu wa usalama katika eneo hilo.

Hata hivyo Jeshi la Polisi lilifanikiwa kulidhibiti kundi hilo na kurejesha hali ya utulivu kwa wakazi wa eneo hilo. 
 
 
Top