Mbunge wa Viti Maalum CUF, Magdalena Sakaya.
Kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Jiji la Tanga, kimevunjika mara tatu mfululizo kutokana na madiwani wa Chama cha Wananchi (CUF) na wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kufanyiana vurugu na kukunjana kutaka kuzichapa kavu kavu.Vurugu hizo zimetokana na uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Tanga kuendelea kumtambua na kumwita katika vikao vya Baraza la Madiwani wa jiji hilo aliyekuwa Diwani wa Kata ya Malungu (CUF), Mohamed Mwambeya, wakati alishajiondoa katika chama hicho.
Mwambeya ambaye alipata udiwani wa kata hiyo kupitia CUF, Agosti, mwaka jana, alitangaza kukihama chama hicho na kuhamia CCM wakati wa mkutano wa Mwenyekiti wa Taifa wa Jumuiya ya Wazazi CCM, Abdallah Bulembo alipofanya ziara mkoani Tanga.
Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano Tanzania, nafasi zote za kuchaguliwa za kisiasa kwa maana ya rais, ubunge na diwani, ni lazima atokane na chama cha siasa na masharti hayo pia yapo katika uchaguzi wa serikali za mitaa.
Hivyo kutokana na katiba hiyo, Mwambeya ambaye alitangaza kujiondoa CUF na kujiunga CCM ni wazi kuwa udiwani wake utakuwa umekoma na msimamizi wa uchaguzi alistahili kutangaza kuwa kata hiyo ipo wazi ili kufanyike mchakato wa kuchagua diwani mwingine atakayetokana na chama cha siasa.
Wakati wa kikao cha jana, vurugu zilizuka baada ya madiwani wa CUF kupinga Mwambeya kuhudhuria kikao hicho hali iliyosababisha polisi kuingilia kati na askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) cha Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga kutuliza vurugu kisha kikao kuahirishwa.
Vurugu hizo zilianza saa 3:00 asubuhi baada ya Meya wa Jiji hilo, Omar Gulled, kufungua kikao hicho.
Baada ya Meya Gulled kuingia kwenye ukumbi wa jiji hilo, madiwani hao walisimama na kupiga makofi na hata baada ya kuketi madiwani wa CUF waliendelea kugonga meza mfululizo, hivyo kikao kushindwa kuendelea na kuahirishwa kwa nusu saa.
Baadaye madiwani waliingia tena ukumbini kwa lengo la kuendelea na kikao hicho badala yake yalianza malumbano ya kutupiana maneno ambayo nusura madiwani wa CUF na CCM wazichape.
Wakati hali hiyo ikiendelea, Diwani Mwambeya anayetuhumiwa kuendelea kuhudhuria vikao hivyo kupitia CUF, alinyanyuka kwenye kiti chake na kwenda kumpora gazeti Diwani wa Viti Maalum wa CUF na kulichana hali iliyosababisha kuzuka zaidi kwa vurugu kwenye ukumbi huo.
Licha ya Meya Gulled kuingia kwa mara ya pili kuendesha kikao cha baraza hilo, aligonga mwamba kwa sababu hakukuwa na maelewano kutokana na madiwani hao kuendelea kugonga meza na kusababisha kuvunjika kwa mara ya pili.
Vurugu hizo zimesababisha halmashauri hiyo kushindwa kuendesha vikao saba kama hivyo tangu kutokea kwa tukio hilo kama hilo la Mwambeya kujiondoa CUF lakini wakati huo akiendelea kuitwa katika vikao vya Baraza la Madiwani.
Akizungumza baada ya kuvunjika kwa kikao hicho, Diwani wa Kata ya Ngamiani Kusini (CUF), Mussa Mbaruku, alisema wamefanya vurugu hizo ili kupinga halmashauri hiyo kuendelea kumtambua Diwani wa Kata ya Marungu, Mohamed Mwambeya kama mwakilishi wa kata hiyo kwa chama hicho wakati alikihama na kujiunga na CCM tangu mwaka jana.
Mbaruku ambaye pia ni Mwenyekiti wa Madiwani wa CUF alisema Mwambeya alitangaza kujiunga na CCM kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Tangamano ambao ulihutubiwa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM Taifa, Bulembo.
Alisema kwa mujibu wa Sheria ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) ibara ya 21 (1-2), sababu za diwani kupoteza nafasi yake ikiwamo kuhama chama kilichompa uongozi.
“Ibara ya 41 (1) ya sheria hiyo inataka apewe barua na Ibara ya 41 (2) Waziri wenye dhamana anatakiwa kutangaza nafasi hiyo kuwa wazi baada ya siku 90... sasa ni zaidi ya miezi sita kuna nini hapa?” Alihoji Mbaruku.
Alidai vurugu wanazozifanya ni moja ya njia ya kufikisha ujumbe kwa halmashauri hiyo na kwa Waziri mwenye dhamana kwa kupitia kikao hicho badala ya kuandamana barabarani.
Madiwani hao walimtupia lawama Meya wa Jiji hilo wakidai anatumika kutekeleza matakwa ya CCM na kwamba amekuwa mzigo kuleta maendeleo ya wakazi wa jiji hilo kutokana na kutofanyika kwa vikao vya baraza hilo.
Vilevile walilaani kitendo cha kuitiwa polisi wakisema ni ushahidi wa kukisaidia CCM kwani kanuni haziwaruhusu askari hao kuingilia shughuli za mabaraza hayo na hatua hiyo ni ya kuwatisha.
Meya Gulled alipohojiwa na NIPASHE kuhusiana na tukio hilo, alielezea kusikitishwa na kuwataka madiwani hao kufuata kanuni, taratibu na sheria badala ya kufanya vurugu.
Alisema baada ya tukio la diwani huyo, kwa nafasi yake amewajibika kwa kumuandikia barua Waziri wa Tamisemi kwenye dhamana kwa sababu siyo wajibu wake wa kuchukua hatua dhidi yake.
Meya huyo alisema athari za vurugu hizo ni pamoja na kutofanyika vikao vya baraza ambavyo ndiyo dira na mwongozo wa halmashauri hiyo kuleta maendeleo kwa wananchi.
Kwa upande wake Mwambeya akizungumzia vurugu hizo, aliponda madai hayo huku akisisitiza kuwa kuwa yeye ni diwani na mwana-CUF safi, hivyo hayo ni majungu na uoga wa kimadaraka kwa viongozi wa chama hicho.
Alisema hajaitwa na chama chake kuhusiana na tukio hilo na kama ni barua alijibu kueleza kuwa licha ya kujitangaza na kuchukua kadi ya CCM lakini bado ni mwana-CUF kutokana na ukweli kuwa hajairejesha kadi yake popote.
Wakati wa mkutano wa Bunge la 16 na 17, Mbunge wa Viti Maalum CUF, Magdalena Sakaya, alimuuliza Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kuhusu sakata la diwani Mwambeya na kuahidi kuwa atalishughulikia.
Waziri wa Tamisemi, Hawa Ghasia, alipotafutwa azungumzie suala hilo, licha ya kupigiwa simu yake mara kadhaa, ilikuwa ikiita bila kupokelewa.
Na Dege Masoli-Nipashe