Marehemu Bundala akiwa na familia yake.
NI huzuni tupu! Aliyekuwa mhamasishaji kwa nyimbo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), mkazi wa Kijiji cha Nyashimo mkoani Simiyu, Bundala Mayala (72), amekutwa amekufa kwa kunyongwa nyumbani kwake.
Mtoto wa mdogo wa marehemu ambaye hakutaka kutaja jina lake gazetini alisema, mwili wa baba yake mkubwa uligundulika Februari 25, mwaka huu, saa nane mchana ambapo ulikutwa na majeraha kadhaa na alipoitwa daktari kumpima alithibitisha kupoteza maisha kwa kunyongwa.
“Siku hiyo ya mwili kugundulika nilikuwa nakwenda nyumbani kwake baba mkubwa kwa lengo la kumsalimia, lakini nilishtuka baada ya kukaribia kwani nilisikia harufu kali ya kitu kilichooza ikitoka ndani huku mlango ukiwa wazi.
“Nilipofika nilichungulia ndani nikaona mguu wa baba ukiwa umejikunja. Ndipo nikaingia haraka na kumkuta marehemu akiwa chini, ameegemea baiskeli yake huku sehemu kubwa ya mwili ikiwa imevimba.“Nilitoka kwenda kuwauliza majirani ambao nao walibaki wakishangaa kwani hata wao walikuwa hawajamuona kwa siku mbili.
“Hata hivyo, wanakijiji na wananchi wengine walishtushwa sana na kitendo hicho kwani marehemu alikuwa ni chombo muhimu sana ndani ya CCM kutokana na umahiri wake wa kuhamasisha shughuli za chama hicho kwa kutumia kipaji chake cha uimbaji.
“Baada ya hapo, nilikwenda kutoa taarifa kwa uongozi wa kijiji ambapo viongozi walifika, wakawaita wanakijiji wote, mimi nikaelekea kituo cha polisi kutoa taarifa,” alisema mtoto huyo.
HALI YA MWILI
Kijana huyo alisema kifo cha baba yake kinatatanisha baada ya uchunguzi wa daktari kuonesha kuwa mishipa ya shingo yake ilikatika, mbavu ziliumia na sehemu ya kiunoni iliumia huku ulimi akiwa ameung’ata na alimwagiwa maji ya moto kwani alibabuka na sehemu ya nyama ya haja kubwa ilinyofolewa.
Aliendelea kusema kuwa, licha ya polisi kufika nyumbani kwa marehemu lakini mpaka sasa hakuna mtu anayeshikiliwa kwa tuhuma hizo na afisa mmoja wa jeshi hilo ambaye aliomba jina lake lisiandikwe gazetini kwa kuwa si msemaji alisema uchunguzi bado unaendelea.Marehemu alizikwa siku hiyohiyo baada ya kugundulika kufuatia jeshi la polisi kutoa ruhusa.