Ikulu imesema Rais Jakaya Kikwete atasaini Muswada wa Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015, kwa kuwa umepitia taratibu zote. Pia, Ikulu imesisitiza kuwa sheria hiyo ni nzuri na itadhibiti matumizi mabaya ya mtandao.
Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu alitoa taarifa hiyo jana, alipozungumza na waandishi wa habari, Ikulu jijini Dar es Salaam. Rweyemamu alisema sheria ya Makosa ya Mtandao itasainiwa na rais muda wowote.
“Hii ni sheria nzuri, kwanza inadhibiti matumizi mabaya ya mitandao, wote watakaohusishwa ama kutuma au kutumiwa vitu au picha mbaya sheria itawabana wote, na kama umetumiwa bila idhini yako, toa taarifa polisi, ili uwe kwenye upande salama,” alisema Rweyemamu.
Alisema madai ya wadau kwamba inanyima uhuru wa kupata taarifa, hayako sahihi kwa kuwa hiyo si sheria ya habari.
Alisema kutokuwa na sheria hiyo, si jambo jema kwa usalama wa nchi.
Muswada wa Sheria ya Makosa ya Mtandao ulipitishwa katika mkutano wa 19 wa Bunge, uliofanyika Dodoma hivi karibuni.
Katika mjadala, wabunge wengi walikemea vitendo vilivyokithiri vya uhalifu wa mtandao nchini, na kutaka sheria hiyo itakaposainiwa, itumike ipasavyo kudhibiti.
Wabunge wengi walisema viongozi, watu maarufu na jamii kwa ujumla, wamekuwa waathirika wakubwa wa matumizi hayo mabaya ya mtandao, kutokana na kutukanwa, kutishiwa kuuawa, kuzushiwa uongo na hata wakati mwingine kutapeliwa.
Hata hivyo, baada ya kupitishwa muswada huo, kumekuwapo na kauli za ukosoaji kutoka kwa watu binafsi na makundi mbalimbali, wakitaka rais asisaini hadi baadhi ya vifungu virekebishwe.
Miongoni mwa mambo yaliyokosolewa ni pamoja na sheria kubana pia mtu anayetumiwa vitu au picha mbaya . Wakati huo huo, Rweyemamu akizungumzia Muswada wa Sheria ya Takwimu kuhusu maombi ya wadau ya kutaka ziangaliwe pande zote mbili wakati wa kutiwa hatiani, kutokana na kutoa au kuandika takwimu zisizo sahihi. Alisema maombi hayo yatazingatiwa.
Kuhusu Muswada wa Sheria ya Habari, uliopelekwa pia katika mkutano wa Bunge uliomalizika hivi karibuni, Rweyemamu alisema;
“Mimi naomba wadau wa habari wauunge mkono muswada huu, madai kuwa umepelekwa bungeni chini ya hati ya dharura sio kosa, na pia madai kuwa haujajadiliwa na wadau nalo sio sahihi, kwani muswada huu umejadiliwa zaidi ya miaka 10, na mimi pia nilishiriki kwenye moja ya mkutano wa wadau kuujadili miaka hiyo pale Morogoro.”
Aidha alisema kuendelea kupinga muswada huo ni kusababisha kuendelea kuwa na sheria ya zamani, jambo ambalo linafanya kukosa sheria mpya. Alisisitiza wadau wa habari kuunga mkono .
Ugaidi
Akizungumzia masuala ya ugaidi, Mkurugenzi huyo wa Mawasiliano Ikulu alishukuru vyombo vya habari kwa kuandika na kuripoti habari za ugaidi kwa kuhabarisha wananchi mbinu za kujihami, iwapo tukio hilo litatokea.
Aliomba viendelee kuhabarisha umma taarifa za kujenga na kujihami dhidi ya matukio hayo, bila kuongeza chumvi na ushabiki.
“Navishukuru vyombo vya habari vimefanya kazi yao ya kuhabarisha umma kuhusu masuala ya ugaidi na mbinu za kujihami, ila kuna baadhi wamekuwa wakiandika habari hizo kwa ushabiki na kuongeza chumvi, jambo ambalo siyo zuri,” alisema.