Mashirika ya misaada yalisema ugonjwa wa kipindupindu na magonjwa mengine yamelipuka kwa maelfu ya wakimbizi kutoka Burundi ambao wamefurika katika kijiji kimoja nchini Tanzania kilichopo pembeni ya ziwa Tanganyika. Ofisi ya kamishna mkuu kwa Shirika la kuhudumia wakimbizi katika Umoja wa Mataifa iliripoti Jumapili kwamba wakimbizi wasiopungua saba wa Burundi walifariki kutokana na kuharisha kupita kiasi.
Ripoti ya Dina Chahali, Dar Es Salaam, Tanzania
Shirika la afya Duniani-WHO lilisema kati ya watu 500 na 2,000 wanawasili kila siku katika kijiji cha Kagunga. Wakimbizi hao wamekimbia nchini mwao kwa sababu ya khofu ya ghasia za kisiasa kufuatia uchaguzi wa mwezi Juni ambao Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza anataka kuwania awamu ya tatu. Uamuzi wake umeibua maandamano kwa wiki tatu katika mji mkuu wa Burundi, Bujumbura na kusababisha fujo ambapo baadhi ya maafisa wa jeshi walijaribu kufanya jaribio la mapinduzi wiki iliyopita ambalo lilishindikana ndani ya muda wa siku mbili.
Waandamanaji wanaompinga Nkurunziza, May 13, 2015.
WHO ilisema katika taarifa yake kwamba kijiji cha kagunga kina wakazi 11,382 kutokana na ongezeko la wakimbizi dadi ya watu na ni zaidi ya 90,000 tangu mwezi April mwaka huu. Hakuna maji salama ya kutosha kwa ajili ya kunywa.
Kulingana na taarifa ya kamati ya kimataifa ya uokozi-IRC ni kwamba kijiji cha Kagunga kimezungukwa na milima hivyo basi wakimbizi lazima wasubiri boti ambayo ni chakavu yenye takribani miaka 100 na kusafiri kwa muda wa saa tatu kuelekea kwenye bandari ya Kigoma. Boti hiyo inasafirisha abiria 600 mara mbili kwa siku na kupelekea msongamano kwa watu wa nyuma na kuwepo hali ya mazingira yasiyo safi.
IRC ilisema ilitoa huduma ya madawa kwa wakimbizi wa kagunga waliopo kwenye boti na wale waliopo kwenye kambi ya muda mkoani Kigoma. Baada ya kufika Kigoma wakimbizi wasiopungua 16,000 wamekwenda kwenye kambi nyingine ya Nyarugusu, safari inayowachukua hadi saa nne kwa kesi za wagonjwa waliopatikana na kipindupindu na kuharisha, kwa mujibu wa WHO.
Rais Pierre Nkurunziza, May 17, 2015.
Wakati huo huo waandamanaji katika mji mkuu wa Burundi, Bujumbura walisema wataendelea kuandamana hadi Rais Pierre Nkurunziza aachie madaraka mwishoni mwa muhula wake wa pili.
Katiba ya Burundi inasema rais anaweza kuchaguliwa kuongoza nchi kwa awamu mbili za muhula wa miaka mitano. Nkurunziza anasema kuwa anaweza kuwania awamu ya tatu kwa sababu bunge lilimchagua kuongoza nchi kwa awamu ya kwanza. Wapinzani wanasema awamu ya tatu inakiuka katiba na mkataba wa Amani wa Arusha, Tanzania ambao ulimaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 2006.