Kufunga ni jambo kongwe na linafanywa na wafuasi wa dini mbalimbali na makundi mengine ya watu. Sababu za kufunga ni nyingi, miongoni ni kufuata mafundisho ya dini au ushauri wa daktari. Wiki hii Waislamu wameanza kufunga Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Wafungaji hao wanajizuia kula kwa takriban saa 14, kuanzia saa 11 alfajiri mpaka saa 12.30 jioni. Wafungaji katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani wana milo mikubwa miwili, mlo wa futari na ule wa daku. Mlo wa futari ni ule ambao mfungaji anautumia ili kufungua kinywa mara tu jua linapozama.
Kwa kuwa mtu amekaa muda mrefu bila ya kula chakula, ni vema futari yake iwe mlo laini ambao ni rahisi kusagwa tumboni. Pia, vyakula hivyo viwe vitamu kutokana na sukari iliyomo katika vyakula vyenyewe.
Tende, maziwa, maji, chai, uji, juisi ya asili, ndizi zilizoiva na kupikwa, magimbi, maboga, viazi vitamu, maharage na mihogoni baadhi ya vyakula laini vinavyofaa kutumika kama futari.
Tende ina asilimia 60 mpaka 70 ya sukari aina ya glukozi na fructose. Mtu akila tende aina hii ya sukari inanyonywa na utumbo na kuunguzwa na seli na hatimae inatoa nguvu kwa haraka. Kwa mfungaji saumu, nguvu hii humpa furaha na akili yake inatuama kwa haraka.
Tende ina protini asilimia 2.5 na madini asilimia 2.1. Pia, ina mafuta kiasi kidogo (asilimia 0.4) ili kukidhi haja ya mwili na haina aina mbaya ya mafuta inayoitwa lehemu.
Zaidi ya hayo, tende ina nyuzi lishe asilimia 3.9%. Nyuzi lishe zinanyonya sumu kutoka tumboni na zinasaidia mtu kupata choo kikubwa mara kwa mara hivyo ananusurika na tatizo la kukosa choo na ugonjwa wa kansa ya utumbo. Tende pia ina vitamini za aina mbalimbali.
Mlo wa futari lazima uwe mlo kamili, wenye mafungu yote ya vyakula kama vile wanga, mafuta, protini, madini, vitamini, maji ya kunywa na nyuzi lishe (dietery fibles).
Kwa hiyo, futari ya mihogo au viazi lazima iwe na maharage, nyama, samaki au dagaa. Vilevile, lazima futari hiyo iwe na matunda na mboga za majani za kutosha.
Vyakula vya futari na daku visiwekwe sukari, chumvi wala mafuta mengi. Mafuta yanayotokana na mimea na kwa kiasi kidogo. Mawese, alizeti, ufuta, mahindi ni miongoni mwa mafuta bora kabisa kwa afya ya mlaji.
Vyakula vyenye chumvi nyingi au vinywaji aina ya koka, chai na kahawa na vile vyenye sukari nyingi viepukwe au vitumiwe mara chache usiku wa Ramadhani.
Vyakula na vinywaji hivyo humfanya mfungaji kupoteza maji mengi panapo kucha kwa njia ya mkojo. Hali hiyo ni hatari kiafya.
Daku ni chakula kinacholiwa usiku wa manane kwa ajili ya kujiandaa kufunga siku inayofuata. Vyakula vizuri kwa daku ni vile vinavyokaa tumboni kwa muda mrefu (kiasi cha saa 6 - 8). Mfano wa vyakula hivyo ni ngano, shahiri, mtama, mahindi, mchele, maharage na kunde.
Vilevile, nyama, samaki, maji ya kunywa, matunda na mboga za majani lazima ziwe sehemu ya mlo wa daku.
Mama mjamzito, mama anayenyonyesha, wagonjwa wa kisukari, wenye Virusi Vya Ukimwi (VVU) na wazee wanatakiwa kupata ushauri kwa wataalamu kabla ya kuanza kufunga.