Mbunge wa Jimbo la Ngara,mkoani Kagera anayemaliza muda wake Bw Deogratius Ntukamazina amewataka Wakazi wa Ngara hususani Wanaume kuondokana na fikra kuwa Wanawake hawawezi kuongoza.
Bw Ntukamazina ametoa kauli hiyo jana katika Mkutano wa Uchaguzi wa Madiwani wa Viti Maalum kupitia Chama cha Mapinduzi uliofanyika kwenye Ukumbi wa Halmashauri ya wilaya ya Ngara.

Amesema baadhi ya wanaume wilayani Ngara Mkoani Kagera wamekuwa na Mtazamo hasi kuhusu uwezo wa Wanawake kuongoza jambo alilodai kuwa ni aina ya ubaguzi kwa Wanawake.

Bw Ntukamazina amesema katika Bunge linalomaliza muda wake wapo wanawake wengi walioonesha uwezo mkubwa katika utendaji wao huku akitolea Mfano wabunge wawili wanaotokea Mkoani Kagera ambao ni Prof Anna Tibaijuka na Bi Asumpta Mshana.

Mbunge wa sasa,Ndugu Deogratius Ntukamazima ambaye amesema kwamba hata gombea tena Ubunge wa jimbo la Ngara akihitaji kupumzika kutokana na kulitumikia taifa kwa muda mrefu.

Katika mkutano huo,Jumuiya ya Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi, UWT wilayani Ngara Mkoani Kagera ilifanya Uchaguzi wa Kuwapata Madiwani wa Viti Maalum ambapo wanawake 7 wameshinda kwenye Uchaguzi huo kati ya 14 waliokuwa wakigombea.

Akitangaza matokeo ya Uchaguzi huo Katibu wa CCM wilayani Ngara Bw Jacob Makune amewataja walioshinda kuwa ni Bi Catherine Edwardkutoka Tarafa ya Murusagamba, Bi.Georgia Mnyonyela wa Tarafa ya Nyamiaga, Bi.Suzana Bahati wa Tarafa ya Rulenge pamoja na Bi Oliver Bugoke kupitia Tarafa ya Kanazi

Katibu huyo wa CCM wilayani Ngara amesema Waliopata nafasi hiyo kwa upande wa Kapu ni Bi Rehema Sadick, Bi.Zawadi Cosmas na Bi Vaileth Vedasto

Bw Makune amewataka madiwani hao kuhakikisha wanashirikiana na wagombea Udiwani kupitia Chama hicho ili wapate ushindi kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 mwaka huu kwa ajili ya kuwatumikia wakazi wa wilaya ya Ngara.

Source:-Radio Kwizera FM.
 
Top