Ewe mtanzania mwenye vigezo vya kupiga kura unatakiwa kutumia haki yako y a kikatiba ya kumchagua kiongozi unayeona anafaa kukuongoza kwa miaka mitano ijayo bila kujari chama cha kiongozi huyo. Ni wajibu wako kuwapima viongozi wote bila ushabiki ili kujua yupi atafaa kuongoza taifa lako. Labda kwa wale ambao hawajui vigezo vikuu vya kuwa mpiga kura ni vema nikagusia kidogo vigezo vya msingi sana kabla ya kwenda kupiga kura.
Ili kuwa na vigezo ya kupiga kura inatakiwa uwe na umri kuanzia miaka 18 na kuendelea na uwe umejiandikisha kwenye daftari la wapiga kura na kupatiwa kitambulisho cha mpiga kura kilichotolewa na tume ya taifa ya uchaguzi (NEC). Pia ni muhimu uwe umehakiki jina lako kwenye daftari hilo kama limo na ni sahihi.
Siku ya kupiga kura yaani hiyo tarehe 25/10/2015 hakikisha unabeba kitambulisho cha na kitunze vizuri hadi utakapofika eneo lako la kupiga kura, msimamizi wa kituo ataomba kuona kitambulisho chako usisite kumpatia maana ni moja ya kuhakikisha kuwa wewe ni raia mwenye sifa wa kupiga kura katika kituo hicho, baada ya kuhakikiwa utapewa karatasi tatu za mgombea udiwani, mgombea ubunge na mgombea urais, ila kwa wale ambao walijiandikisha kata tofauti na mahali kituo cha kupigia kura kilipo watapatiwa karatasi mbili yaani ya mgombea ubunge na mgombea urais. Vivyo hivyo kwa wale waliojiandikisha jimbo tofauti la uchaguzi na mahali kituo cha kupigia kura kilipo watapewa karatasi moja yaani ya mgombea uraisi tu.
Mambo ya kuzingatia ukiwa kwenye chumba cha kupigia kura, hakikisha unaangalia vizuri jina la kiongozi uliyechagua kuwa anafaa kukuongoza, kisha angalia sehemu ya kichumba cha kuweka alama ya vema (tick) kama ishara ya kumchagua kiongozi wako, hakikisha alama ya vema inatosha tuu kwenye kichumba hicho usiweke mbwembwe kiasi cha kuzidisha urefu wa tick hadi nje ya kichumba hicho maana hapo kura yako itakuwa imeharibika, pia usiandike maneno kwenye karatasi ya kura kufanya hivyo utaharibu kura yako.
Ewe mtanzania linda na dumisha amani ya nchi yetu epuka makundi ya uvurugaji na yenye nia ya kuchafua uchaguzi huu, kura yako ndo maamuzi yako ee mungu ibariki Tanzania.