Wanafunzi watatu wa shule ya Sekondari Kanazi wilayani Ngara Mkoani Kagera wamefariki huku wengine 19 wakijeruhiwa baada ya kupigwa na radi wakiwa shuleni.
Mganga wa Zamu katika Hospitali ya Murugwanza, walikokimbizwa Majeruhi hao Dr Edwin Ngeze amesema wanafunzi hao watatu wamefariki muda mfupi baada ya kufikishwa kwenye Hospitali hiyo kutibiwa majeraha na kwamba kati ya waliofariki ,Wasichana ni wawili na Mvulana mmoja.

Imeelezwa kuwa tukio hilo limetokea Jana ,February 10,2016, majira ya Saa Nane mchana muda mfupi baada ya Wanafunzi hao kutoka kwenye viwanja vya michezo na kukimbilia madarasani kwa ajili ya kujikinga Mvua ambapo ghafla ilipiga radi na kuwajeruhi.

Dr Ngeze amesema wanaendelea kuwahudumia majeruhi hao na kwamba taarifa rasmi itatolewa baada ya uchunguzi kufanyika katika miili yao.

Akizungumza katika Hospitali ya Murugwanza walikolazwa Majeruhi hao na kuhifadhiwa Miili ya waliofariki, Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wilayani Ngara, Bi Honoratha Chitanda amesema Serikali itawagharamia matibabu waliojeruhiwa na kushiriki maziko ya waliofariki.


 
Top