Paul Makonda 
Kwa ufupi

12,562-Idadi ya walimu wa shule za msingi mkoani Dar es Salaa.
4,285-Idadi ya walimu wa shule za sekondari jijini Dar es Salaam
Sh270m-Kiasi cha fedha ambacho walimu hawatalipa kwenye daladala iwapo mpango huo utatekelezwa kwa mwezi.
Sh800-Wastani wa nauli ya mwalimu mmoja kwa siku kwa kima cha chini. Wakati baadhi ya walimu wametoa maoni tofauti kuhusiana na ofa ya kusafiri bure katika mabasi ya daladala jijini Dar es Salaam, imebainika wamiliki wa mabasi, kwa siku watakosa kiasi cha Sh13.4 mpango huo utakapoanza kutekelezwa.

Ofa ya usafiri wa bure kwa walimu wa shule za msingi na sekondari zinazomilikiwa na Serikali ilitangazwa juzi na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda mbele ya viongozi wa vyama vya usafirishaji abiria na madereva Mkoa wa Dar es Salaam.

Katika tangazo lake Makonda alisema kuanzia Machi 7, walimu wa shule za Serikali za msingi na sekondari mkoani Dar es Salaam hawatalipa nauli kwenye daladala wakati wakienda na kutoka kazini.

Makonda alisema wazo lake, ambalo awali lililenga walimu wa wilaya yake ya Kinondoni, limeungwa mkono na viongozi wa vyama vya wasafirishaji abiria na wamiliki wa daladala na kwamba kilichobaki ni kuanza kutoa huduma hiyo.

Makonda aliagiza wakuu wa shule za msingi na sekondari kuanzia jana kuwatengenezea walimu wao vitambulisho kwa ajili ya usafiri huo.

Maoni ya walimu

Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, baadhi ya walimu hao walisema kinadharia mpango huo ni mzuri, lakini utasababisha udhalilishaji watakapoanza kutumia vitambulisho kama tiketi ya kuingia kwenye mabasi.

Mwalimu mkuu wa Shule ya Msingi Mapambano, Amina Msangi alisema anahofia udhalilishwaji wanaofanyiwa wanafunzi kutokana na kulipa nusu nauli, utahamia kwa walimu ambao watakuwa wakisafiri bure.

“Kama umewahi kupanda daladala, lazima umeshuhudia wanafunzi wanavyonyanyasika; kusukumwa nje kwa kuwa tu wanalipa nusu nauli. Sasa itakuwaje kwa sisi ambao hatutalipa kabisa?” alihoji.

“Nafikiri Serikali ingeboresha maslahi yetu kwanza, maana maisha yetu yataonekana duni sana. Wapo watakaofikiri hawa walimu wanafanya nini hapa mjini, itashusha taaluma, hadhi na haitawavutia vijana wanaomaliza masomo kujiunga ualimu,” alisema.

Mwalimu mwingine kutoka Shule ya Msingi Mzimuni alimpongeza mkuu wa wilaya kufikiria suala hilo, lakini alisema hofu yake ni ugumu katika utekelezaji wake.

“Kwa nini wasiboreshe mishahara yetu na ndani yake kukawa na posho za usafiri na nyumba kama sekta binafsi badala ya kutaka tusafiri bure? Wafanye hivyo na sisi tutanufaika,” alisema mwalimu huyo aliyeomba jina lake lisitajwe gazetini.

“Maisha ya walimu wa Dar es Salaam yanakuwa duni kwa kuwa shule nyingi hazina nyumba za walimu na usafiri ni shida kutoka eneo moja kwenda jingine.”

Meneja Utafiti na Uchambuzi wa Sera wa Hakielimu, Godfrey Bonaventure alisema suala la walimu kutumia vitambulisho kupanda daladala ni kuwaongezea kero ya kugombana na makondakta na hivyo kuishia kudharaulika.

Alisema walimu bado wana changamoto nyingi, hivyo kumsaidia kupanda daladala ni kitu kidogo kwake. Alisema kinachotakiwa ni kuboresha maisha ya mwalimu na maslahi yake kwa kuwa asipolipa nauli kwenye daladala ataokoa Sh30,000 tu kwa mwezi,” alisema.

“Kuna changamoto nyingi zitakuja katika hili, mishahara yao ni midogo sana,” alifafanua.

“Leo unaondoa nauli ambayo ni Sh800 au Sh1,000, hapo huwezi kuwa umemsaidia chochote zaidi ya kumuongezea kero ya kwenda kugombana na makondakta,” alisisitiza.

Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Ezekiah Oluoch alisema wasiwasi wake ni kwamba hakuna uhakika kama suala hilo limeshirikisha hata mabasi yaendayo kasi.

Alisema pia fedheha kwa walimu inaweza kuwa changamoto kubwa ambayo watakabiliana nayo na inaweza kuwafanya washindwe kutekeleza majukumu yao shuleni.

“Kuwe na mkataba wa kisheria. Lisiwe tamko la kisiasa ili iwapo Makonda ataondoka katika kitengo hicho, suala hilo libaki hivyo hivyo na hata ikiwa Mkuu wa Mkoa Meck Sadiki atahama libaki katika maandishi,” alisema Oluoch.

Lakini baadhi ya makondakta wa mabasi ya abiria jijini Dar es Salaam, wamepongeza hatua hiyo iliyofikiwa na Makonda, wakisema itasaidia kuboresha maisha ya walimu. Kondakta wa daladala linalofanya kazi kati ya Gongo la Mboto na Mnazi mmoja, Sunday Salum alisema iwapo wanafunzi wataendelea kulipia nauli, haoni tatizo walimu kupanda bure.

“Serikali wenyewe wameshaangalia kwa mapana na marefu, wamejua kwamba haitaleta madhara kwetu,” alisema Sunday.

Kondakta wa daladala inayosafiri kati ya Tabata Segerea na Mnazi Mmoja, Idrisa Ally alisema iwapo mamlaka zimeshakubaliana basi wao hawana neno. “Kwa mtazamo wangu itasaidia, mimi nina vijana wawili wanasoma shule ya msingi, hawa walimu wanaelimisha jamii na watoto wetu, sisi makonda tuna elimu tumefundishwa na wao litakuwa jambo zuri,” alisema.

CHANZO: MWANANCHI

 
Top