Halmashauri ya Jiji la Tanga ipo hatarini kuvunjwa kufuatia madiwani wake kushindwa kuelewana katika kikao kilichositishwa leo na Mkurugenzi mtendaji. 
Kikao hicho cha baraza la madiwani wa Halmashairi ya Jiji la Tanga kwa mujibu wa barua za mwaliko walizopewa madiwani hao kilikuwa ni cha mwendelezo wa mkutano wa Desemba 19 mwaka jana ambacho pia kilivunjika baada ya kutokea vurugu. 

Chanzo cha kuvunjika kikao cha leo ni baada ya diwani wa kata ya Tangasisi (CUF) ambaye pia ni Naibu Meya, Mohamed Haniu kuchukua kipaza sauti na kutangaza kwamba kama wanataka kikao hicho kiendelee ni lazima ufanyike uchaguzi wa Meya. 

“Kwenye wito wa barua za kikao hiki hakuna ajenda ya uchaguzi kwa hivyo tukubaliane kwanza kwamba tunaanza na uchaguzi wa Meya ndipo tuendelee kwa sababu hatuna meya hadi sasa”alisema Haniu. 

Tangazo hilo lilisababisha madiwani wa kutoka chama cha wananchi (CUF) kushangilia jambo lililomlazimu Meya wa Jiji, Mohamed Mustapha (Selebosi) kutamka kwamba kikao anakiahirisha. 

Tamko la Selebosi lilisababisha madiwani wa CUF kushangilia kwa mara ya pili huku wakiimba nyimbo za kukisifu chama hicho. 

Baada ya kuahirishwa kwa kikao hicho,Meya wa Jiji hilo, Mohamed Selebosi, Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Abdullah Lutavi, Mbunge wa Jimbo la Tanga, Mussa Mbarouk na Kaimu Mkurugenzi wa Jiji, Dk Wedson Sichalwe waliingia katika ofisi ya Mkurugenzi kufanya kikao chao cha ndani. 

Akizungumza na waandishi wa habari,Kaimu Mkurugenzi , Sichalwe alisema ajenda ambazo zilikuwa zijadiliwe ni kuunda kamati za kudumu za halmashauri, kupanga ratiba za vikao vya halmashauri, kupokea taarifa ya utendaji wa halmashauri katika kipindi ambacho madiwani hawakuwepo na kupokea taarifa ya Serikali. 

“Kama mlivyoshuhudia kikao kimevunjika,inapotokea vurugu kama vile hakuna sababu ya kuendelea na kikao, sheria inamruhusu Meya kukivunja” alisema Dk Sichalwe na kusisitiza kuwa taarifa zaidi atatoa baadaye. 

Diwani wa Kata ya Duga (CUF), Halid Rashid alisema watakuwa tayari kuendelea na kikao iwapo madiwani wa CCM watakubali uchaguzi wa nafasi ya meya ufanyike upya kwa sababu hawamtambui Mohamed Mustafa kama Meya. 

“Ni bora Halmashauri ya jiji ivunjwe kama Serikali inalazimisha tumtambue Selebosi kuwa ni Meya, sisi hatutakubali akae mbele kuongoza kikao aje huku ndiyo kikao kiendelee” alisema Halid. 

Mohamed Haniu (CUF) alisema anaamini Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martin Shigela anaweza kumaliza mgogoro wa nafasi ya Meya wa Tanga kwa kutumia busara ya kuamuru uchaguzi wa meya ufanyike upya. 

Diwani wa kata ya Chumbageni (CCM) Saida Gaddafi aliwataka madiwani kutoka chama cha CUF kukubali matokeo yaliyomtangaza Selebosi kuwa Meya kwa sababu hata wao walimkubali Mohamed Haniu kuwa Naibu Meya. 

Mkuu wa Wilaya ya Tanga aliwahimiza madiwani wa Jiji kukubaliana ili vikao vya kupitisha miradi ya maendeleo ya wananchi viweze kuendelea. 

Dalili za kutokea vurugu katika kikao hicho zilijitokeza mapema kufuatia jeshi la polisi kumshikilia Mwenyekiti wa CUF Wilaya ya Tanga na aliyekuwa mgombea wa nafasi ya Meya wa jiji la Tanga, Rashid Jumbe asubuhi kabla ya kuanza kikao hicho. 

Taarifa za kushikiliwa na jeshi la Polisi diwani huyo zilienea na hata kikao kilipoanza hakuwepo ukumbini ambapo madiwani wenzake walisema alikamatwa kwa madai ya kuratibu shughuli za matangazo kuhusiana na kikao hicho kwa kutumia gari lililopita mitaani. 

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga,Leonard Paul alithibitisha kukamatwa kwa diwani Rashid Jumbe na kwamba alikuwa akituhumiwa kutangaza mitaani kwa kutumia gari kuhusu kikao hicho.
 
Top