Mahakama ya Wilaya ya Kigoma imemhukumu Sheikh wa Msikiti wa Goma, Hassan Bamba (48), kifungo cha miaka 30 jela, baada ya kukutwa na hatia ya kubaka. 
Sheikh huyo alifikishwa mahakamani hapo kwa tuhuma za kumbaka mwanafunzi wa darasa la sita katika Shule ya Msingi Kitongoni, mwenye umri wa miaka 14 na kumsababishia maumivu makali sehemu za siri. 

Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu wa Mahakama hiyo, Frola Mtariania, baada ya upande wa mashtaka kuthibitisha kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo. 

Hakimu Frola, akitoa hukumu hiyo, alisema mahakama inatoa adhabu kali dhidi ya mshtakiwa ili iwe fundisho kwake na kwa viongozi wengine wenye tabia ya kikatili kama yake. 

Alisema upande wa mashtaka ulipeleka mashahidi watano, pamoja na kielelezo cha PF3, ambacho kilithibitisha kwamba Sheikh Bamba mshtakiwa alitenda kosa hilo. 

Alipotakiwa kujitetea ili kupunguziwa adhabu, akiongozwa na wakili wa kujitegemea Method Kabuguzi, mshtakiwa aliangua kilio na kuiomba mahakama impunguzie adhabu kwa sababu ana familia inamtegemea. 

Pia alidai ni kosa lake la kwanza tena shetani alimwingilia. Hakimu Frola alitupilia mbali utetezi huo na kusema: 

"Mshtakiwa ukiwa kiongozi wa dini, kitendo ulichokifanya si cha kijamii maana wewe ndiwe unayefundisha watu kuachana na maovu cha kushangaza unakuwa ndiye wa kwanza kuyatenda maovu. 

"Sasa utakwenda gerezani miaka 30 ili ukajifunze tabia ya kuwa kiongozi bora wa dini, kwa sababu huku uraiani umeshindwa kuishi na jamii." 

Awali, akisoma hati ya mashtaka, Wakili wa Serikali Anita Julius, alidai kuwa Januari Mosi, mwaka huu, saa 4 asubuhi eneo la Ujiji Kigoma, mshtakiwa huyo alibaka msichana huyo. 

Ilidaikwa kuwa siku ya tukio mtoto aliyebakwa akiwa na pacha wake, ambao baba yao ni rafiki wa sheikh huyo, walikwenda kwa sheikh huyo kwa ajili ya kuombewa duwa na kufanyiwa dawa kwa ajili ya kufaulu mtihani wa kuingia darasa la saba. 

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, baada ya kufika, Bamba alimtuma mwenzake aende shuleni kuchukua mchanga na ndipo alipomfanyika kitendo hicho yule aliyebaki. 

Mwenzake aliporejea, ilidaiwa kuwa alimkuta pacha wake analia na alipomuuliza alimjibu kuwa amebakwa na Bamba. 

Umati mkubwa wa wakazi wa Manispaa ya Kigoma/Ujiji, wakiwamo waumini wa msikiti aliokuwa akiswalisha, ulikusanyika mahakamani na kushuhudia Sheikh huyo anapelekwa jela.
 
Top