Mkazi wa Kitongoji cha Kapembo, Kijiji cha King’wangoko wilayani Kaliua, Mkoa wa Tabora, ametiwa mbaroni akituhumiwa kumuua, mama yake mzazi , Kiziko Lukambwe kwa kumnyonga kisha kumtundika ndani ya nyumba waliyokuwa wakiishi. 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Hamis Issa alisema kijana huyo anatuhumiwa kumnyonga mama yake na kumning’iniza ndani ya nyumba, ili ichukuliwe kuwa amejinyonga. 

Issa alieleza kuwa uchunguzi unaendelea kubaini chanzo cha mauaji hayo na kwamba, polisi wanamshikilia mtuhumiwa kwa mahojiano zaidi. 

Alionya wanaofanya uhalifu hawatapata nafasi ya kukimbia mkono wa sheria. 

Majirani wa Kiziko, walieleza kwamba mwanamke huyo amekuwa akilalamika kuwa haelewani na mtoto wake. 

“Kiziko inaelekea hakuwa na uhusiano mzuri na mwanaye kwa vile alikuwa akilalamika kuwa, hawaelewani,” alisema mkazi wa Kona nne, Yuda Ngati. 

Wilaya ya Kaliua ina matukio mengi ya mauaji yatokanayo na sababu mbalimbali, ikiwamo ulipizaji visasi na imani za ushirikina. 

Kamanda Issa aliwataka wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi na kwamba, Serikali haitawavumilia watu wa aina hiyo. 

Pia, alitaka kamati za ulinzi na usalama za vijiji kuimarisha ulinzi kwa kushirikiana na askari na kwamba, polisi peke yao hawawezi.

CREDIT: MALUNDE 1 BLOG
 
Top