Mmoja wa wahisani wa kanisa la Anglikana Dayosis ya Kagera kutoka kisiwa cha Gumsey nchini Uingereza Paul Smith akimtwisha ndoo ya maji Jovina John mkazi wa kijiji cha Kasharaza wilayani Ngara mkoani Kagera baada ya kutembelea mradi wa maji jana akiambatana na wenzake kutoka nchini Canada.

Baadhi ya wafadhili kutoka nchini Uingereza na Canada kupitia kanisa la Anglikana Dayosisi ya Kagera, wakifurahia matumizi ya fedha zao za kujenga miradi ya maji wilayani Ngara ambapo jana walitembelea kisima cha maji cha kijiji cha Kasharazi wilayani humo.
Picha na habari kwa Hisani ya Shaaban Ndyamukama



Kanisa la Anglikana dayosisi ya Kagera limejenga visima vya maji 16 kwa mwaka 2016 katika vijiji mbalimbali wilayani Ngara vyenye thamani ya Sh 90.6 milioni ili kuwapatia wananchi huduma ya maji safi kuwaepusha na magonjwa ya matumbo baada ya kutumia maji ya mito na madimbwi wilayani humo


Visima hivyo vimefadhiliwa na Marafiki wa kanisa hilo kutoka nchini Canada na Uingereza ambapo wananchi huchangia asilimia 20 ya rasilimali zinazowazunguka ikiwa ni pamoja na kutumia nguvu zao kujenga visima hivyo kwa kushirikisha kamati za maji na serikali za vijiji .


Mratibu wa mfuko wa Tumaini ulio chini ya kanisa la Anglikana wilaya ya Ngara Bw Alex Nyamkara, amebainisha hayo jana wakati wafadhili wa kanisa hilo walipotembelea miradi ya maji katika vijiji vya Kasharazi, Nyamahwa, Nyakisasa, Kibirizi na Kanyinya wilayani Ngara.


Bw.Nyamkara alisema ujenzi wa kisima kimoja hugharimu Sh 5.64 milioni na kwamba wananchi wengi hutumia maji ya mito na madimbwi kwa kuchanganyikana na wanyama wa aina mbali mbali na kusababisha magonjwa ya matumbo, kuharisha na homa za vipindi kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano.


Alisema kata ambazo zimenufaika na miradi ya maji kupitia kanisa hilo ni Ntobeye, Muganza Nyamiaga, Bukiriro, Mbuba, Nyakisasa , Kibogora na Kanazi na kwamba mfuko wa tumaini hutoa mafunzo kwa wajumbe wa kamati za maji ili kuhifadhi vyanzo na mazingira vinapojengwa visima kwa kukarabati miundombinu ya maji


Aidha alisema kwa mwaka huu wameomba wafadhili kuwaongezea fedha za kujenga visima 13 katika kata zenye mahitaji makubwa ya maji kama Keza, Murusagamba, Rusumo,Kasulo na Kabanga ili kuwawezesha wananchi kupata unafuu wa huduma baad ya miradi ya maji ya Benki ya dunia kukwama kukamilika


“Tunachohimiza wananchi ni kutunza miradi ya maji kwa kuwa ni mali yao si ya Tumaini Fund na ikiboreshwa wanaweza kunufaika nayo kwa muda mrefu na kuwashawishi wafadhili kuwaongezea miradi mingine” Alisema Nyamkara


Wakati huo huo alisema wafadhili hao walitoa fedha za kuwajengea nyumba wajane na wagane wanaoishi na watoto yatima katika mazingira magumu ambapo na mwaka jana zilijengwa nyumba 28 zenye thamani ya Sh 70 milioni na mwaka mwaka huu zitajengwa nyumba 17 zenyethamani ya Sh 42.5 milioni.


Hata hivyo mmoja wa wafadhili wa kanisa hilo kutoka nchini Canada, Linda Winey aliwahimiza wachungaji na waumini mbalimbali katika vijiji alivyotembelea kumtumainia Mungu kwa kufanya kazi kwa bidii wakitumia juhudi na maarifa ili kuboresha maisha yao.


Wafadhili hao walisema walitembelea wilaya ya Ngara katika shughuli za kiroho lakini wananchi wa Tanzania wanakabiliwa na ugumu wa maisha hivyo kunahitajika uboreshaji wa muiundombinu na mazingira katika utoaji huduma bora za kijamii hasa maji, Afya, elimu na makazi kwa wasiojiweza kiuchumi.


CREDIT: MWANAWAMAKONDA.BLOGSPOT.COM
 
Top