WAKURUGENZI wawili wa Kampuni za Saha Limited na Lucky Shipping Co.Ltd, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashitaka mawili ya uhujumu uchumi ikiwemo kupeperusha bendera ya Tanzania bila kibali.
Washitakiwa hao ni Issa Haji au Salum (39) ambaye ni baharia na Mkurugenzi wa Kampuni ya Lucky Shipping pamoja na Abdullah Hanga (73) mfanyabiashara na Mkurugenzi wa Kampuni ya Saha ambaye ni mkazi wa Mbezi Beach.
Akisoma mashitaka hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Victoria Nongwa, Wakili wa Serikali, Wankyo Saimon alidai washitakiwa walijihusisha na mtandao wa uhalifu kinyume na aya 4(1) C, jedwali la kwanza na kifungu cha 57(1) na 60 (2) cha Sheria ya Uhujumu uchumi.
Saimon alidai kuwa Julai 19, mwaka jana na Januari 16, mwaka huu jijini Dar es Salaam, walitoa ushauri, msaada na maelekezo katika kutenda kosa la jinai la mtandao wa uhalifu ambalo ni kupeperusha bendera ya Tanzania kwenye meli iitwayo Huihang 68 zamani ilijulikana kama Greko 02, bila kuwa na hati ya usajili kutoka kwa msajili wa meli nchini kwa lengo la kujipatia faida kutoka katika shughuli za uvuvi haramu.
Pia alidai kuwa Julai 19, mwaka jana na Januari 16, mwaka huu, katika jiji la Dar es Salaam washitakiwa hao huku wakifahamu kuwa ni kosa kisheria waliruhusu upeperushwaji wa bendera katika meli hiyo ya Huihang 68 au zamani ilijulikana kama Greko 02 bila kuwa na leseni kutoka kwa msajili wa meli kwa lengo la kuifanya ionekane kuwa ya Tanzania wakati sio kweli.
Hakimu Nongwa alisema washitakiwa hao hawatakiwi kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo.
Hata hivyo, Saimon alidai kuwa upelelezi wa shauri hilo upo katika hatua za mwisho kukamilika hivyo wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kuieleza mahakama taarifa za upelelezi huo.
Wakili wa utetezi, Dismas Raphael aliiomba mahakama ijielekeze katika Katiba ambayo inawatambua washitakiwa hao kama watuhumiwa na kwamba iwatendee haki kwa kuwapatia dhamana.
Akijibu hoja hiyo, Saimon alidai kuwa Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP), amewasilisha hati ya kuzuia dhamana kwa washitakiwa hao kwani wakipewa dhamana wataingilia maslahi ya Taifa hivyo mahakama ijielekeze katika suala hilo.
Pia alidai Ibara ya 59 (B) ibara ndogo ya 3 inaainisha mamlaka ya DPP kuhusu masuala yote yanayolenga maslahi ya Taifa kama ilivyoainishwa kwenye Katiba.
“Kama upande wa utetezi wanalenga kuipinga hati ya kuzuia dhamana wanatakiwa wafuate taratibu nyingine katika mahakama za Kikatiba ambapo watakapowasilisha maombi yao, sisi tutayajibu ndipo mahakama itatoa maamuzi,” alidai Saimon.
Hakimu Nongwa alisema upande wa utetezi uwasilishe mapingamizi yao kuhusu hati hiyo na upande wa mashitaka ujibu na kwamba mahakama hiyo itatoa maamuzi kama hati hiyo ni sahihi au la.
Hata hivyo, aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 22, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa na kwamba washitakiwa hao wamerudishwa rumande.