MVUA kubwa imenyesha mkoani Mwanza na kusababisha maafa, ikiwemo vifo vya watu wawili na familia kadhaa kukosa makazi kutokana na nyumba kubomoka.
Aidha, mvua hiyo imesababisha kufungwa kwa muda uwanja wa ndege wa Mwanza kutokana na kujaa maji.
Mvua hiyo inasadikiwa ndiyo mwanzo wa El-Nino kutokana na taarifa ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kueleza jana kwamba, kutakuwa na mvua za El-Nino, kama ilivyokuwa imeelezwa katika taarifa yake ya Septemba mwaka huu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Charles Mkumbo katika mkutano wake na waandishi wa habari, alisema mmoja wa waliopoteza maisha, ni mwendesha bodaboda wa Kirumba aliyekuwa amepakiza wanafunzi wawili akiwapeleka shuleni.
Kuhusu wanafunzi hao, Kamanda alisema, taarifa zake hazijathibitishwa kama pia wao wamepoteza maisha, ingawa tukio hilo limo katika orodha ya athari za mvua hizo.
Alisema mtu mwingine alionekana akiwa anaelea katika maji eneo la Mabatini, lakini baadaye mwili wake haukuonekana kutokana na mafuriko hayo.
“Tumepokea taarifa juu ya mvua hizi kutoka maeneo mbalimbali ya jiji la Mwanza na tunaendelea kukusanya taarifa na kuchukua hatua stahiki,” alisema Kamanda Mkumbo.
Kuhusu uwanja wa ndege, mvua hizo zilisababisha kufungwa kwa saa tano kwa uwanja wa ndege wa Mwanza baada ya kujaa maji.
Meneja wa uwanja wa Ndege wa Mwanza, Esther Madale alimwambia mwandishi wa habari kwamba uwanja huo ulilazimika kufungwa kwa saa tano kwa ajili ya kuwezesha wahandisi, kufanya uchunguzi wa miundombinu yake.
Hakuna ndege iliyoruhusiwa kutua katika muda huo. “Ni kweli tulikumbwa na mkasa huo wa mvua ambazo zilinyesha mfululizo na kusababisha kufungwa kwa uwanja kwa muda…kwa sasa tunavyoongea tayari huduma zimerejea katika hali yake ya kawaida,” alisema Madale.
Uwanja huo wa ndege upo katika matengenezo makubwa, ikiwamo mnara wa kuongozea ndege, njia za kurukia ndege ambazo sasa ni meta 2000 na zinaongezwa hadi kufikia meta 3300. Ukarabati huo ulianza mwaka 2012 na ulitarajiwa kumalizika Oktoba mwaka huu.
El-Nino imeanza
Katika taarifa ya TMA kwa vyombo vya habari jana, ilisema kuendelea kuongezeka kwa joto katika maeneo ya Bahari ya Pasifiki kunaonesha kuimarika kwa mvua za El-Nino kama ilivyoelezwa katika taarifa iliyotolewa Septemba, mwaka huu.
Taarifa hiyo iliyosainiwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA, imesema mvua zimeshaanza kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini hususani Ukanda wa Ziwa Viktoria, Kanda ya Magharibi na Nyanda za Juu, Kaskazini Mashariki na zinataraji kuwa za juu ya wastani.
“Hata hivyo, mifumo mingine ya hali ya hewa ikiwemo mwitikio wa mfumo ya hali ya hewa katika Bahari ya Hindi imekuwa na mchango hasi kinyume na ilivyotarajiwa katika mwenendo wa mvua za Vuli nchini katika kipindi cha mwezi Oktoba, 2015 na kusababisha vipindi virefu vya upungufu wa mvua katika mikoa ya Morogoro, Pwani na Dar es Salaam,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Aidha taarifa hiyo ya Dk Chang’a ilisema maeneo yanayopata mvua mara moja kwa mwaka mikoa ya Dodoma, Singinda, Ruvuma, Lindi, Mtwara, Songea, Mbeya, Iringa, Njombe, Tabora, Kigoma Rukwa na Katavi mvua zinatarajiwa kuanza kati ya wiki ya pili na ya nne ya Novemba, 2015.
Alisema mvua hizo zimeanza kujiimarisha katika mikoa ya Kigoma, Tabora na Katavi na zinatarajiwa kusambaa katika maeneo mengine mwezi huu. Hata hivyo, wilaya za Kondoa, Kongwa na Singida Vijijini katika mikoa ya Dodoma na Singida, zinatarajiwa pia kupata vipindi vya mvua mwanzoni mwa mwezi huu.
Mamlaka hiyo imeshauri wananchi, hususani wafugaji, Mamlaka za Wanyamapori, Mamlaka za Maji na Afya waendelee kutafuta, kupata na kufuata ushauri wa wataalamu katika sekta husika katika kutekeleza mipango inayoweza kuathiriwa na mwelekeo wa hali ya hewa iliyotabiriwa. Aidha mamlaka imetaka wananchi na wadau kwa ujumla kuzingatia hadhari mbalimbali zilizokwisha kutolewa.
Taarifa hiyo imesema mwelekeo wa mvua uliotolewa umezingatia zaidi viashiria vya mvua katika kipindi cha msimu (miezi mitatu) na hali ya mvua katika maeneo makubwa.
Hivyo, viashiria vinavyochangia mwenendo wa mifumo ya mvua na mabadiliko ya muda mfupi katika maeneo madogo utazingatiwa katika uchambuzi wa utabiri wa muda wa kati na mfupi.
TMA imeahidi kuendelea kufuatilia mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na kutoa taarifa za mwelekeo wa mvua nchini.