Waziri wa Kilimo, Uvuvi na Ufugaji Mh. Mwigulu Nchemba leo hii amefika Mvomero kijiji cha Dihinda kata ya Kanga kufuatilia na kuchukua hatua dhidi ya tukio baya la mauaji na kujeruhi binadamu na wanyama lililotokea Desemba 12/2015
Akizungumza na wananchi hao Waziri Mwigulu Nchemba alikuwa na haya ya kusema
"Natoa rai kwa Wananchi hususani wa jamii ya Wafugaji na Wakulima, hakuna ardhi au mnyama mwenye thamani sawa na maisha ya mwanadamu yeyote yule,njia bora na salama ya kutatua migogoro hii inayohusisha wakulima na wafugaji ni kufuata taratibu za kuonana na uongozi wa serikali wa eneo husika hatua kwa hatua". Alisema Mh. Mwigulu
Pia Mh. Mwigulu amesema ameagiza ulinzi maeneo yote yenye migogoro, pili wahakikishe waliosababisha maafa wanakamatwa mara moja na kufikishwa kwenye vyombo vya sharia. na Kwa walio jeruhiwa, ameagiza wapatiwe matibabu kwanza bila kuchelewa na hatua za kisheria kwa wenye hatia zifuate.
"Nawaomba wananchi waache kujichukulia sheria mikononi, tunakwenda kuunda kamati za usuluhishi wa migogoro hii kwa kila kijiji zitakazohusisha pande zote mbili ili kubaini wavamizi wa maeneo na kuwachukulia hatua za kisheria."